IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
15:30 - May 15, 2019
News ID: 3471958
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hakutakuwa na vita baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuingia vitani na Marekani licha ya kushtadi taharuki baina ya pande mbili na kusisitiza kuwa, Washington inafahamu vyema kuwa, kuingia katika vita na Tehran hakutakuwa na maslahi yoyote kwake.

Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo jana Jumanne mjini Tehran, wakati alipokutana na wakuu wa mihimili mitatu ya serikali, wabunge pamoja na shakhsia wengine wa ngazi za juu wa kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi hapa nchini amesisitiza kuwa, "Makabiliano kati ya Iran na Marekani hayatakuwa ya kijeshi. Hakuna vita vyovyote vitakavyofanyika."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza bayana kuwa: Chaguo la msingi kwa taifa la Iran mkabala wa Marekani ni muqawama au mapambano na kusimama kidete, na katika mapambano hayo, hatimaye Marekani italazimika kusalimu amri.

Ayatullah Khamenei amefafanua kuwa, "Kutokana na vitisho vya Washington, chuki ya Wairani dhidi ya Marekani imeongezeka zaidi ya mara kumi."

Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran amesisitiza kuwa, vikosi vote vya jeshi la Iran viko tayari na viko macho kuzima chokochoko za maadui wakati huu kuliko wakati wowote ule.

Katika sehemu nyingine katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefutilia mbali pia uwezekano wa kufanyika mazungumzo kati Tehran na Washington kutokana na kile alichokitaja kama mienendo na sera za uhasama na uadui za Marekani kwa taifa hili.

Amesema, "Hakuna afisa yeyote wa Iran mwenye hekima atakubali kufanya mazungumzo kuhusu uwezo mkubwa wa taifa hili; kufanya mazungumzo na serikali ya sasa ya Marekani ni 'sumu hatari yenye kuangamiza'."

Sambamba na kuashiria namna sera za Marekani kwa Ulaya na Asia zimegonga mwamba, Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa jamii ya Wamarekani inakabiliwa na changamoto za kiuchumi na kijamii, kutokana na uongozi mbaya na malumbano ya kila siku miongoni mwa maafisa wa serikali ya Washington.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha malengo ya kikhabithi ya Marekani ya kutaka kubadilisha mahesabu na kuwafanya viongozi wa Iran wasalimu amri mbele yake pamoja na kuwaweka mbali wananchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Katika mapambano na adui kuna njia mbili tu hakuna ya tatu; nazo ni imma sisi kurudi nyuma na kuruhusu maadui kusonga mbele au kusimama kidete na kuendelea na muqawama. Uzoefu wetu unaonesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu popote tunaposimama kidete kukabiliana na adui huwa tunafanikiwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Matatizo makubwa ya kijamii, migongano na uporomokaji mkubwa ndani ya serikali ya Marekani ni uhakika ambao unaonesha jinsi adui anavyozidi kuwa dhaifu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa ushahidi wa jambo hilo kutoka katika ripoti rasmi za taasisi za serikali ya Marekani akisema: Kuweko Wamarekani milioni 41 wanaosumbuliwa na matizo ya umaskini na ukosefu wa usalama wa chakula, kuweko asilimia 40 ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa, kuweko wafungwa milioni mbili na laki mbili, (kiwango ambacho ni kikubwa zaidi cha wafungwa kulingana na jamii za nchi zote duniani), kuweko idadi kubwa ya Wamarekani wanaotumia mihadarati na madawa ya kulevya na kuweko asilimia 31 ya mashambulizi ya kupigana risasi katika jamii ya Marekani (kiwango ambacho ni kikubwa mno ikilinganishwa na nchi nyingine zote duniani), ni miongoni mwa mambo ambayo yanaonesha sura halisi ya Marekani. Ameongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu wanadhani kuwa Marekani ni nchi kubwa sana yenye ubabe na hatari mno mtu kuweza kukabiliana nayo, (lakini uhakika hauko hivyo) na tab'an hatupaswi pia kughafilika na vitendo vya adui.

Vile vile amegusia malengo na masharti ya Marekani katika mazungumzo na hasa suala la nguvu za makombora za Iran akisisitiza kuwa, nchi hiyo ya kibeberu inaitaka Iran ipunguze masafa yanakofika makombora yake na ustadi wake wa kupiga shabaha ili itakapofika siku ya kutumiwa, makombora hayo, yasiweze kutekeleza ipasavyo malengo yaliyokusudiwa. Ameongeza kuwa: Ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba hakuna mtu yeyote nchini Iran anayekubaliana na jambo hilo. Tunapolizingatia jambo hilo tutaona kuwa kitendo chenyewe tu cha kufanya mazungumzo na Marekani ni kosa kwani kufanya mazungumzo na nchi hiyo ambayo haiheshimu kitu chochote; si masuala ya kimaadili wala ya kisheria na wala mambo yanayokubaliwa na watu wote duniani, ni jambo lisilo na maana kabisa.

3811631

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: