IQNA

20:34 - June 21, 2019
News ID: 3472009
TEHRAN (IQNA)- Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo Tehran ameashiria hatua ya kutunguliwa ndege isiyo na rubani (drone) ya Marekani ambayo ilikuwa imekiuka anga ya Iran na kusema: "Wakuu wa Marekani wafahamu kuwa, Lango Bahari la Hormoz daima litakuwa kaburi la wavamizi."

Hujjatul Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari katika hotuba zake za Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameongeza kuwa, Wamarekani wamechanganyikiwa baada ya Iran kutungua drone yao ya kijasusi na kuongeza kuwa: "Awali rais wa Marekani alikakanusha kuangushwa drone na kisha baadaye akakiri. Jambo hilo linaonyesha kuwa amechanganyikiwa."

Hujjatul Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari amesisitiza kuwa, Iran katu haitaanzisha vita lakini iwapo adui ataanzisha vita dhidi ya Iran, basi afahamu kuwa hataweza kuvimaliza vita hivyo.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran pia ameashiria uwezo wa Iran wa kujihami na kusema: "Ili kukabiliana na vitisho vya adui, Iran ina uwezo mkubwa sana wa kumzuia adui na kwa msingi huo Wamarekani wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa kuhusu chokochoko zao."

Hujjatul Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari amesisitiza kuwa, Marekani inapaswa kuliomba radhi taifa la Iran kutokana na hatua yake ya kukiuka anga ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha amesisitiza ulazima wa kuishtaki Marekani katika taasisi za kimataifa.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amebaini kuwa tawala vibaraka wa Marekani katika eneo zinapaswa kusitisha ujinga wa kununua silaha za Marekani.

Amesema tawala hizo za Kiarabu zinapaswa kufahamu kuwa, drone ya kijasusi ambayo Wamarekani walikuwa wanadai kuwa haiwezi kuonekana kwenye rada huku wakiinadi kuwa iliyo ya kisasa zaidi duniani, imelengwa na kutunguliwa kwa ustadi mkubwa na makombora yaliyotengenezwa nchini Iran.

Alkhamisi alfajiri, ndege moja ya kijasusi isiyo na rubani ya Marekani aina ya RQ-4 Global Hawk ilitunguliwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika pwani ya kusini mwa Iran mkoani  Hormozgan  katika eneo la Lango Bahari la Hormoz katika Ghuba ya Uajemi baada ya kuingia kinyume cha sheria katika anga ya Iran. Kitengo cha angani cha IRGC kimeonysha mabaki ya drone hiyo Ijumaa mjini Tehran.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Iran imetoa za mfumo wa kiimataifa wa GPS, drone hiyo ya kijasusi ya Marekani ilikuwa katika anga ya Iran wakati wa kutunguliwa. Marekani haijaweza kutoa ushahidi wowote wa maana kuthibitisha madai yake.

3821125

Name:
Email:
* Comment: