IQNA

23:55 - July 15, 2019
News ID: 3472045
TEHRAN (IQNA) - Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran wameandamana kulalamikia kuendelea kushikiliwa kushikiliwa kinyume cha sheria Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Wanachuo wa vyuo vikuu hapa mjini Tehran leo wamefanya mkusanyiko mkubwa kulalamikia kuendelea kushikiliwa korokoroni Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Wakiwa wamebeba mabango na maberamu, wanachuuo hao walisikika wakipiga nara za kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky. Sambamba na kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, wanachuo hao wamelaani vikali kimya cha jamii ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria.
Aidha wanachuo hao kutoka vyuo vikuu mbalimbali hapa mjini Tehran wameitaka serikali ya Nigeria kumuachilia huru mara moja, kiongozi huyo wa Waislamu wa Kishia.
Kadhalika wanachuo hao, wameitaka Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran kufanya kila iwezalo ili kuhakikisha Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa kwa miaka kadhaa sasa anaachiliwa huru.
Kwigineko Jumuiya ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Kidini katika mji wa Qum nchini Iran wamelaani hatua ya serikali ya Nigeria kuendelea kumshikilia kinyume cha sheria Sheikh Zakzaky.
Katika taarifa, Jumuiya ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Kidini katika mji wa Qum nchini Iran imesema utawala wa Nigeria unabeba dhima ya afya ya Sheikh Zakzaky. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, utawala wa Nigeria unamtendea unyama Sheikh Zakzaky kwa uungaji mkono wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na utawala wa Saudia Arabia. Aidha Tarrifa hiyo imesema Nigeria na waitifaki wake hao wa kigeni wamempa sumi Sheikh Ibrahim Zakzaki ili kuzidi kuwashinikiza Waislamu.
Sheikh Zakzaky na mkewe walitiwa mbaroni tarehe 13 Disemba 2015 katika Huseiniya ya Harakati ya Kiislamu huko Zaria kufuatia shambulio la jeshi la nchi hiyo lililoua shahidi mamia ya Waislamu wasio na hatia.
Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru mara moja mwanachuoni huyo mwezi Disemba 2016 na kuliwajibisha jeshi la nchi hiyo kuilipa familia ya Sheikh Zakzaky fidia ya dola laki moja na 50 elfu.
Hata hivyo jeshi, serikali na vyombo vya dola vya Nigeria vimekataa kabisa kutekeleza amri hiyo ya mahakama na hadi hivi sasa mwanaharakati huyo wa Kiislamu anaendelea kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria.
Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashtaka.
Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo.

/3468960

Name:
Email:
* Comment: