IQNA

15:46 - August 21, 2019
News ID: 3472093
TEHRAN (IQNA) – Waislamu wanakamatwa kiholela katika viwanja vya ndege na vituo vya mpakani Uingereza kwa visingizio vya ugaidi katika kile kinachoonekana ni sera rasmi ya chuki dhidi ya Uislamu.

Kwa mujibu wa taasisi ya haki za binadamu ya Cage, kuna ongezeko kubwa la ushahidi unaoonyesha kuwa Waislamu wanazuiwa kwa masaa kadhaa katika viwanja vya ndege na vituo vya mpakani bila sababu huku wanawake Waislamu wakilazimishwa kuvua Hijabu.

Cage imesema imewasilisha malalamiko rasmi katika Idara Huru ya Utendaji Kazi wa Polisi Uingereza kwa niaba ya waathrika 10 na pia imewaandikia barua wabunge kuhusu vitendo vya kuwabagua Waislamu,

Mkurugeni wa Cage, Adnan Siddiqui, amesema makumi ya maelfu ya watu wamekuwa wakisimamishwa bila sababu na asilimia 0.007 tu ndio hupatikana na makosa.

Muingereza mmoja ambaye alijitambulisha kwa jina lake la kwanza, Omer, amesema amesimamishwa asilimia 95 ya mara zote ambazo amekuwa akiwa anarejea kutoka Ubelgiji, Ufaransa na Italia.

Maafisa wa usalama  Uingereza wamekuwa wakitumia kipengee cha 7 cha sheria ya ugaidi ya mwaka 2000 ambayo inawaruhusu maafisa wa usalama kumzuia msafiri mpakani hadi masaa sita iwapo anashukiwa kuhusika katika vitendo vya ugaidi.

Kila anayekamatwa hana haki ya kukaa kimya, anapaswa kukabidhi polisi simu au computer na paswadi mbali na maafisa wa usalama kuchukua alama zake za vidole na vipimo vya vinasaba DNA.

Kwa mujibu wa sensa ya hivi karibuni ya watu Uingereza, kuna Waislamu milioni 2.8 nchini humo kati ya watu milioni 64 nchini humo. Waislamu wameenea katika maeneo yote ya Uingereza na wamewakilishwa katika sekta zote za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Pamoja na hayo kunashuhudiwa ongezeko la  vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika jamii, sekta binafsi na serikalini.

3469216

Tags: iqna ، Waislamu ، Uingereza
Name:
Email:
* Comment: