IQNA

23:21 - September 27, 2019
News ID: 3472149
TEHRAN (IQNA) - Vyama vya Kiislamu nchini Sudan vimelaani mpango wa serikali ya mpito ya nchi hiyo wa kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel.

Kwa mujibu wa taarifa, Murtadha al Toum, Katibu Mkuu wa muungano wa vyama vya Kiislamu unaojulikana kama 'Uungaji Mkono wa Sharia za Kiislamu na Serikali ya Kisheria', ametoa wito kwa Wasudan kushiriki katika maandamano ya kulaani mpango huo wa serikali ya mpito. Amesema ni wazi kuwa mpango huo ni katika sera jumla za serikali ya mpito kuleta mfumo wa kisekulari nchini humo.
"Tutasimama kidete kupunga hatua hizo," alisisitiza wakati akihutubia waandishi habari hivi karibuni mjini Khartoum.
Mwanaharakati maarufu Mohamed Abdul Karim amesema mwamko wa watu wa Sudan mwezi Disemba, ambao ulipelekea kutimuliwa madarakani Omar al Bashir, haukuwa na lengo la kuleta usekulari nchini humo.
Ameongeza kuwa wananchi wa Sudan ni Waislamu wenye imani thabiti na hivyo hawatakubali Uislamu uhujumiwe.
Kufuatia maandamano makubwa ya wananchi wa Sudan,mwezi Aprili mwaka huu Jeshi la Sudan lililazimika kumuondoa madarakani al Bashir ambaye alikuwa ameitawala nchi hiyo kidikteta kwa muda wa miaka 30.
Kufuatia mazungumzo baina ya makundi ya kiraia na wanajeshi, Baraza la Utawala wa Mpito la Sudan liliundwa mwezi Agosti na linaongozwa na wajumbe 11 wakiwemo sita wa kiraia na wanajeshi watano; na litaongoza kwa muda wa miaka 3 kuelekea uchaguzi mkuu.

3844778/

Name:
Email:
* Comment: