
Kwa mujibu wa ripoti ya IQNA, Muhammad Hussein Abulhassan, mchambuzi wa Kiarabu aliandika katika tovuti ya Taghyeer utawala wa Kizayuni wa Israel unavyohusika katika kuchochea machafuko ya Sudan: "Wakati fulani, Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Golda Meir, alisema: “Kudhoofisha mataifa makubwa ya Kiarabu na kuondoa nguvu na uwezo wao ni jukumu na ni lazima ili kuongeza nguvu ya Israel katika kukabiliana na maadui wake. Hii inahitaji wakati mwingine kutumia nguvu, diplomasia na vita vya siri.”
Kauli hii inaonyesha juhudi za Tel Aviv za kuyumbisha mataifa ya Kiarabu kutoka ndani kwa kutumia udhaifu wa kijamii, ambapo mifano dhahiri ni Iraq na Sudan.
Njama hii ilianza zamani; Israel, ikizingatia umuhimu wa kimkakati wa Sudan kwa Misri, ilifanikiwa kuigawa Sudan kuwa nchi mbili mwaka 2011 na bado inaendelea kujaribu kuigawa zaidi pamoja na mataifa mengine. Baada ya uvamizi wa 1967, hasa katika mkutano wa Khartoum, Sudan iligeuzwa kuwa kituo cha mafunzo na makazi ya vikosi vya anga na nchi kavu vya Misri. Kutokana na hali hiyo Israel ikaamua kutekeleza njama ya kuigawa Sudan kuwa vipande vipande. Njama hiyo imetekelezwa kwa kuchochea vita vya ndani ili kuizingira Misri, kupanua ushawishi wa Kizayuni–Kimarekani katika vyanzo vya Mto Nile na kuyumbisha usalama wa kitaifa wa Waarabu.
Israel inachochea machafuko Darfur
Avigdor Dichter, waziri wa zamani wa 'ulinz'i wa ndani wa Israel, amefichua kuwa taarifa za kijasusi za Israel zilichochea mapigano ya Darfur ili kuisukuma hali kuelekea kwenye mgogoro na mgawanyiko zaidi.
Alibainisha kuwa mapigano ya sasa nchini Sudan hatimaye yataishia kwa kugawanywa nchi hiyo katika nchi kadhaa ndogo ndogo. Dichter ndiye aliyetoa tathmini na mipango ya Israel ya kuchochea migawanyiko nchini Lebanon, Syria, Iraq, Iran, Sudan, Libya, Algeria, Saudi Arabia na Misri (ambayo ni lengo kuu).
Tangu Israel ilipofanikiwa, kwa kushirikiana na Ethiopia na wengine, kuichochea Sudan Kusini ijitenge na Kaskazini, imekuwa na uwepo wa kificho katika uwanja wa Sudan.
Pia Israel ilipanga njama ya kuzuia mradi wa Jonglei Canal ambao ungeweza kuokoa mabilioni ya mita za ujazo za maji kwa Sudan na Misri badala ya kupotea kwa uvukizi na mabwawa. Sasa Israel, kwa kushirikiana na wengine, inachochea vita vya Sudan ili kuigawa nchi hiyo, ikitekeleza nadharia ya “ipe vita nafasi” ya Edward Luttwak, msomi wa Kizayuni, kwa kuchochea migawanyiko ya kikabila.
Waasi wa RSF
Kwa kuanza kwa vita vya sasa, waasi wa RSF walianza tena mauaji dhidi ya makabila ya 'Kiafrika' huko Darfur. Wakati jeshi lilipoanza kushinda na kuikomboa mitaa mingi ya Khartoum na kuonekana liko karibu kushinda, sauti za Israel zilianza kusikika ziimtuhumu Sudan kwa kushirikiana na Iran. Kwa msingi huo kukawa na tetesi za kutaka kuingilia moja kwa moja, kwa madai kuwa jeshi la Sudan limekuwa “Hamas ya Afrika.”
Baada ya wanamgambo wa RSF kudhibiti kwa nguvu Darfur na kufungua njia za usafirishaji kupitia Libya, Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Ethiopia, walijiunga na harakati ya Abdulaziz al-Hilu na kutangaza nia ya kuunda serikali katika eneo hilo na sehemu za Kordofan Kusini. Hatua hii ni jaribio la kurudia mfano wa Libya na kuunda serikali mbili hasimu.
Si Vita Kamili, Si Amani Kamili
Hatari ya hali hii ni kuendeleza hali ya “si vita kamili, si amani kamili” nchini humo, hali inayodhoofisha mshikamano wa kijamii na kisiasa na hatimaye kuondoa nguvu za kitaifa. Ikiwa wanamgambo hawa watafanikiwa kudumu kwa muda mrefu, watakuwa chombo cha Israel na nguvu nyingine zinazotaka kujitenga kwa Darfur, nguvu ambazo mipango yao inajulikana wazi.
Mnamo tarehe 5 mwezi huu, Natalia Cuadros, mtafiti wa Kizayuni aliyebobea katika masuala ya Afrika, alichapisha makala katika gazeti la Jerusalem Post akitaka kuondolewa kwa Jenerali Abdul Fattah al Burhan madarakani Sudan. Alidai kuwa ushirikiano wa Burhan na Iran na Ikhwanul Muslimin unageuza Sudan kuwa uwanja mpya dhidi ya Israel.
Madola makubwa ya dunia yanaiaangalia Sudan kama moto karibu na ghala la baruti; hawataki kuuwasha, lakini pia hawana imani na yeyote wa kuuzima. Hatari halisi ni kwamba Sudan inaelekea kusambaratika na kuwa uwanja wa vita vya niaba.
Janga halikuanza leo
Ni wazi kuwa janga hili halikuanza leo. Chanzo chake kilitokana na harakati ya Kiislamu na utawala wa Ikhwan Muslimin chini ya uongozi wa viongozi wa zamani wa nchi hiyo, Hassan Turabi na Omar El Bashir, waliopora madaraka, wakageuza taasisi za taifa kuwa zana za chama na kufungua milango kwa wanamgambo na mamluki wanaomwaga damu ya watu wa Sudan, akiwemo Muhammad Hamdan Dagalo Musa maarufu kwa lakabu Hemedti, ambaye ni kinara wa waasi wa RSF. Madikteta huleta uharibifu na wavamizi huleta maangamizi.
Leo Sudan inahitaji sana kujijenga upya kabla haijageuzwa kuwa uwanja wa vita vya niaba. Kwa kuzingatia mizani ya nguvu, uongozi wa Sudan unapaswa kurekebisha tena uhusiano wake wa kimataifa ili kuzuia na kuondoa mipango hii mibaya kabla ya kuendelea kuharibu rasilimali za taifa. Waarabu na Waafrika kwa pamoja wanapaswa kuchukua hatua na kuacha kupuuza hatari inayoikabili Sudan kisha mshikamano wa Kiarabu katika kuzuia ushawishi wa Israel barani Afrika na kuzuia kugawanywa kwa Sudan.
Ni lazima kuhakikisha kuwa hakuna serikali sambamba itakayokubalika Sudan. Hivyo hatua ya Mohamed Hamdan Dagalo kuapishwa kuwa kiongozi wa serikali sambamba ya Sudan mjini Nyala, Darfur inapaswa kupuuzwa na kulaaniwa.
Juhudi za kumaliza mgogoro
Kunahitajika juhudi za kumaliza migawanyiko ya Kiafrika–Kiarabu, kuzingatia utofauti wa kikabila na kidini katika jamii zao, na kuwasaidia Waafrika wanaoteseka kwa umaskini katikati ya migogoro isiyoisha ambayo Israel inaitumia kupenya katikati ya Afrika na kuchochea vita, na hatimaye kuyafanya mataifa kutegemea misaada yake.
Sudan iko katika njia panda na kulinda umoja wake kunahitaji hekima kubwa. Ni lazima kutambua kuwa vita havitabaki ndani ya mipaka ya Sudan pekee. Damu tayari imeanza kusambaa pande zote. Juhudi zozote za amani zitashindwa maadami waharibifu kama Israel wataruhusiwa kuendeleza uingiliaji na umwagaji damu wa siri na wa wazi nchini Sudan.
4318626