IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kuna siku Wapalestina watarejea katika ardhi zao

10:10 - October 31, 2019
Habari ID: 3472194
TEHRAN (IQNA) –Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kuna siku Wapalestina watarejea katika ardhi zao ambazo sasa zinakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran wakati wa Hafla ya 17 ya Pamoja ya Kuhitimu Maafisa wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Chuo Kikuu cha Ulinzi wa Anga cha Khatamu Anbiya SAW na kuongeza kuwa: " Leo tunaona namna ambavyo madola ya kiistikbari yamegharamika kiasi kikubwa cha fedha katika eneo letu la Asia Magharibi lakini yamefeli na madola hayo yenyewe yanakiri kufeli. Wanasema wamegharamika dola trilioni saba katika eneo na kuambulia patupu. Nukta hii inaonyesha tunaweza kutegemea nguvu ya Mwenyezi Mungu na kuwa na matumaini kuhusu mustakabali. 'Maandamano ya Kurejea', ambayo hufanywa na Wapalestina kila Ijumaa katika Ukanda wa Ghaza hatimaye yataweza kufanikisha lengo la Wapalestina la kurejea katika ardhi zao."

Ayatullah Khamenei amebaini kuwa, kushindwa mutawalia utawala wa Kizayuni mkabala wa vijana wa Hizbullah na vijana wenye hima wa Palestina katika vita vya siku 33, siku 22 na siku saba ni mifano ya wazi ya kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria njama za maadui za kuvuruga usalama katika baadhi ya nchi za eneo na kusema: "Wanaojali Iraq na Lebanon wafahamu kuwa, kipaumbele chao kinapaswa kuwa kuondoa hali ya ukosefu wa usalama na wananchi wa nchi hizo nao wafahamu kuwa, matakwa yao ya haki yanaweza tu kukidhiwa katika fremu ya mfumo wa kisheria." Ameendelea kubaini kuwa: "Wahusika wa ukhabithi na chuki hatari wanajulikana na nyuma ya pazia katika matukio ya sasa ni Marekani na mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi kwa msaada wa kifedha wa baadhi ya tawala zinazopinga mageuzi katika kieneo."

Ayatullah Khamenei amesema pigo kubwa zaidi kwa nchi yoyote ni kuvurugwa usalama wake na kuongeza kuwa: "Maadui walikuwa na dhana hiyo kuhusu Iran lakini taifa angalifu la Iran lilijitokeza katika medani kwa wakati na vikosi vya ulinzi navyo pia vilikuwa tayari na vilisambaratisha njama hizo."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria baadhi ya jinai za majeshi ya Uingereza, Ufaransa na Marekani katika kipindi cha miaka 100 iliyopita huko India, Mashariki na Magharibi mwa Asia, na Kaskazini na Kati mwa Afrika na kusema jukumu kuu la majeshi ya kiistikbari ni uvamizi, ukaliaji mabavu na kuhujumu nchi zingine lakini katika falsafa na mantiki ya majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nukta muhimu ni kulinda ardhi ya nchi kwa nguvu na kujizuia na uvamizi.

3469769/

 

captcha