IQNA

11:30 - November 27, 2019
News ID: 3472233
TEHRAN(IQNA) – Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelalamikia vikali hatua ya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Norway hivi karibuni.

Malalamiko hayo yamekabidhiwa Naibu Balozi wa Norway mjini Tehran ambaye ameitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran siku ya Jumanne.

Idara ya Masuala ya Ulaya Kaskazini katika Wizara ya Mambo ya Nje imemuita balozi huyo na kumkabidhi malalamiko ya Iran kufuatia kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Norway na kuonya kuwa, vitendo kama hivyo vitakuwa na matokeo hatari kama vile kuenea misimamo mikali ya kidini na utumiaji mabavu.

Aidha Iran imesema kitendo kama hicho kilichojaa chuki kimeumiza hisia za Waislamu duniani na kusisitiza kuwa, si sawa kutusi itikadi na matukufu ya Waislamu zaidi ya bilioni 1.5 duniani kwa kisingizio cha uhuru wa maoni. Halikadhalika Iran imeitaka serikali ya Norway ichukue hatua za kuzuia kukaririwa vitendo kama hivyo katika siku za usoni.

Naibu Balozi wa Norway, kwa upande wake, amesema atawasilisha malalamiko ya Iran kwa serikali ya nchi yake na amesisitiza kuwa, serikali ya Norway inapinga kitendo hicho cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu. Amebaini kuwa sera ya Norway ni kuunga mkono uhuru wa maoni na wakati huo huo kuzuia kuenezwa chuku huku akiongeza kuwa, serikali ya Oslo inalipa umuhimu mkubwa suala la usalama wa Waislamu wanaoishi katika nchi hiyo.

Jumapili iliyopita, katika mji wa Kristiansand, wanachama wa kundi linaloupinga Uislamu  linalojiita 'Zuieni Norway kuwa ya Kiislamu' (SIAN) walikichoma moto Kitabu Kitukufu cha Mwenyezi Mungu (Qur'an Tukufu). Kundi hilo la SIAN na lililo dhidi ya Uislamu liliasisiwa mwaka 2000 ambapo lengo lake ni kukabiliana na ongezeko la wafuasi wa dini hiyo nchini Norway. Aidha kundi hilo linadai kwamba, dini ya Uislamu inakiuka katiba ya nchi hiyo kama ambavyo eti inakinzana na matukufu ya kidemokrasia na ubinaadamu.

3859865

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: