IQNA

Iran, Iraq zalaani hujuma dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Najaf

18:18 - November 28, 2019
Habari ID: 3472237
TEHRAN (IQNA) – Serikali za Iran na Iraq zimelaani hujuma dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran katika mji mtakatifu wa Najaf huku serikali ya Iraq ikisema hujuma hiyo imelenga kuvuruga uhusiano wa kihistoria wa nchi hizi mbili jirani.

Siku ya Jumatano, genge la wahuni, waliokuwa wamefunika nyuzo zao, waliuhujumu ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Najaf na kuteketeza moto jengo hilo la kidiplomasia. Aidha walishuhsa bendera ya Iran na kupandisha ile ya Iraq.

Kufuatia tukio hilo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema Alhamisi asubuhi amelaani vikali kushambuliwa ubalozi mdogo wa Iran mjini Najaf, Iraq na kuitaka Baghdad iwachukulie hatua kali wote waliohusika na uhalifu huo.

Sayyid Abbas Mousavi amelaani vikali kitendo cha kihuni kilichofanywa na wafanya fujo hao na kuitaka serikali ya Iraq kuchukua hatua madhubuti za kulinda maeneo ya kidiplomasia na wanadiplomasia. Amesema, balozi wa Iraq hapa Tehran amekabidhiwa rasmi malalamiko makali ya Tehran kuhusu shambulio hilo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq nayo imetoa taarifa na kulaani vikali hujuma hiyo dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran. Taarifa hiyo imesema lengo la hujuma hiyo ni kudhuru uhusiano mzuri na wa kihistoria baina ya Iran na Iraq.

Kabla ya tukio la jana la kushambuliwa ubalozi mdogo wa Iran mjini Najaf, balozi nyingine ndogo za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilishambuliwa katika siku za huko nyuma kwenye miji ya Basra na Karbala na watu waovu wanaotumia vibaya maandamano ya wananchi wa Iraq ya kulalamikia ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira na ufisadi serikalini.

Katika miezi ya hivi karibuni, Iraq imekuwa ikishuhudia maandamano ya watu wanaodai kulalamikia ughali wa maisha lakini maandamano hayo yametekwa na magenge ya wahuni wanaotekeleza uharibifu mkubwa na mauaji.

Ushahidi mbalimbali unaonesha kuwa, maandamano ya wananchi wa Iraq yamechochewa na wageni wasiolipendea kheri taifa hilo na ambao wamekasirishwa na kuangamizwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) lililokuwa limeteka sehemu kubwa za ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

3469984

captcha