IQNA

15:18 - December 15, 2019
News ID: 3472280
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemteua Hujjatul Islam Hamid Shahriyari kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika dikrii amemteua katibu mkuu mpya wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu na kuelezea matumaini yake kuwa, kutapatikana taufiki kwa kuendelezwa jitihada ambazo zimekuwa zikitekelezwa na wasimamizi waliotangulia wa jumuiya hiyo.

Katika dikrii hiyo, Kiongozi Muadhamu amesema: "Alhamdulillah, leo kote katika ulimwengu wa Kiislamu kwa kuwepo busara itokanayo na muongozo wa Mwenyezi Mungu, wasomi, wanaharakati  na wanaotaka mema, kumepatikana hatua endelevu za kukabiliana na fitina, hasa fitina za kimadhehebu."

Amesema nukta hiyo ni kinyume cha sera za makafiri na waistikbari wa kimataifa ambao wanataka kuchochea mivutano baina ya Waislamu  lakini Alhamdulillah, njama zao zimefeli.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema inatazamiwa kuwa, Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu itatumia busara ya Kiislamu pamoja na wanafikra na wasomi katika Ulimwengu wa Kiislamu hasa vijana katika kuchukua hatua za kukukuribisha kifikira na kivitendo madhehebu za Kiislamu na kwa msingi huo kujenga upya harakati iliyoanza miongo kadhaa iliyopita. Aidha kiongozi muadhamu ametoa shukrani zake za dhati kwa katibu mkuu anayeondoka, Hujjatul Islam Muhsin Araki kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wake. 

Inafaa kuashiria hapa kuwa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ilianzishwa mwaka 1990  kufuatia dikrii ya Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuleta umoja, maelewano na ukuruba baina ya madhehebu za Kiislamu. Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu inafuatilia malengo ya Darul Taqrib iliyokuwa Cairo, Misri na ambayo ilididimia baada ya kuaga dunia maulamaa walioiasisi taasisi hiyo ya umoja wa Kiislamu.

3864146/

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: