IQNA

15:30 - October 27, 2020
News ID: 3473300
TEHRAN (IQNA) - Mkutano wa 34 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu unatazamiwa kuanza Alhamisi kwa njia ya intaneti ambapo mada kuu itakuwa 'Ushirikiano wa Kiislamu Wakati wa Maafa na Majanga'.

Akizungumza na waandishi habari hivi leo mjini Tehran, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu Hujjatul Islam Hamid Shahriyari amesema kongamano hilo litaanza Alhamisi na kuendelea hadi Jumanne ijayo yaani tarehe tatu Novemba.

Hujjatul Islam Hamid Shahriyari ameongeza kuwa, Kongamano la 34 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu mwaka huu litakuwa na wazungumzaji 167 wa kigeni kutoka nchi 47 na 120 kutoka Iran. Amesema wazungumzaji ni wanazuoni na wasomi maarufu kutoka ulimwengu wa Kiislamu na wataalamu wa masuala ya umoja na kukurubisha madhehebu za Kiislamu.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema katika kongamano la mwaka huu kutazinduliwa vitabu viwili kuhusu Palestina sambamba na kufunguliwa Radio ya Umoja.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu aidha ameashiria kitendo cha wakuu wa Ufaransa kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na kusema: "Maadui wanahimiza chuki dhidi ya Uislamu na hivyo kuna haja ya kutumia busra na mazungumzo ili kuwasilisha Uislamu halisi duniani na tusiruhusu hao maadui wauarifishe Uislamu ambao si sahihi ambao unahimiza machafuko kwa lengo la kuchafua jina la Uislamu halisi."

Mkutano wa kimataifa wa umoja wa Kiislamu hufanyika kila mwaka kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shiia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

3931472

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: