IQNA

Rais Hassan Rouhani wa Iran
11:51 - December 19, 2019
News ID: 3472287
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ulimwengu wa Kiislamu una changamoto nyingi kitaifa na kimataifa na kusisitiza kuwa, nchi za Kiislamu zinapaswa kuwa na tadibiri na mikakati madhubuti ya kuachana na ubeberu wa sarafu ya dola wa kutegemea mfumo wa kifedha wa Marekani.

Rais Rouhani amesema hayo mapema leo asubuhi wakati wa ufunguzi wa kikao cha viongozi wa nchi za Kiislamu cha "Kuala Lumpur 2019" huko Malaysia na kusema kuwa, changamoto kubwa zaidi zilizopo katika ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa kitaifa na kimataifa ni za utamaduni na utambulisho, kutostawi kimaendeleo na changamoto za kiuchumi.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, hatari za kudhoofika utambulisho wa kitaifa na Kiislamu na kutawaliwa na tamaduni za maajinabi ndilo tishio kubwa zaidi hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ameongeza kuwa, vita katika nchi za Syria na Yemen, machafuko na ukosefu wa utulivu katika nchi za Iraq, Lebanon, Libya, na Afghanistan ni matunda ya kuwepo misimamo ya kuchupa mipaka ya ndani na uingiliaji wa madola ya kibeberu katika masuala ya nchi za Kiislamu.

Rais Rouhani ameongeza kwamba, hakuna kitu chochote kinachoweza kuziba pengo la ushirikiano wa karibu wa nchi za Kiislamu na kusisitiza kuwa, mshikamano na ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi wa nchi za Kiislamu unaweza kuufanya ulimwengu wa Kiislamu kuwa kambi kubwa na madhubuti yenye utajiri mwingi na nguvu kubwa za kielimu na kiteknolojia jambo ambalo litapelekea kutatuliwa matatizo mengi ya Waislamu na kukabiliana ipasavyo na madola ya kibeberu.

Mkutano huo ambao umeanza Alhamisi, umehudhuriwa pia na viongozi wengine muhimu wa ulimwengu wa Kiislamu ambao ni mwenyeji, Waziri Mkuu Mahathir Mohammad wa Malaysia, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani. 

3864993

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: