IQNA

Waziri Mkuu wa Malaysia
10:35 - December 22, 2019
News ID: 3472296
TEHRAN (IQNA) - Waziri Mkuu wa Malaysia Mahathir Mohammad amesema Iran, Malaysia, Uturuki na Qatar zinatafakari kutumia dinari ya dhahabu na mfumo wa bidhaa kwa bidhaa katika biashara.

Akizungumza Jumamosi wakati wa kufunga Kongamano la Kuala Lumpur 2019 katika mji mkuu wa Malaysia, Mahathir amezipongeza Iran na Qatar na kuzitaja kuwa nchi huru na zenye kujitegemea ambazo zinaweza kusimama kidete kukabiliana na vikwazo na mizingiro.

Amesema si Qatar na Iran pekee zinazoathiriwa na vikwazo na mizingiro na kwa msingi huo kuna haja ya nchi za Kiislamu kujitegemea katika siku za usoni ili kukabiliana na vitisho.

Mahathir Mohammad amesema amewahi kupendekeza kuwa nchi za Kiislamu zitumie dinari ya dhahabu badala ya sarafu za kigeni hasa dola ya Marekani na mfumo wa bidhaa kwa bidhaa katika biashara ili kukabiliana na vikwazo.

Kikao cha viongozi wa nchi za Kiislamu cha "Kuala Lumpur 2019" kilianza Alhamisi, na kuhudhuriwa pia na viongozi wengine muhimu wa ulimwengu wa Kiislamu ambao ni mwenyeji, Waziri Mkuu Mahathir Mohammad wa Malaysia, Rais Hassan Rouhani wa Iran, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani.

Saudi Arabia imesusia kikao hicho kwa madai kuwa kinalenga kuvuruga Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC. Aidha Saudia pia imezichochea nchi za Kiislamu kutohudhuria mkutano huo ambao umehudhuriwa na wawakilishi wa ngazi za juu wa nchi 20 kati ya nchi 53 wanachama wa OIC. Hata hivyo Malaysia imekanusha madai hayo ya Saudia. Kikao hicho cha Kuala Lumpur kilijadili masuala muhimu yanayowahusu Waislamu duniani kama vile matatizo ya wakimbizi Waislamu, chakula, utambulisho wa kitaifa na kiutamaduni, chuki dhidi ya Uislamu, teknolojia, biashara, intaneti na usalama.

3470154

 

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: