IQNA

21:33 - January 18, 2020
News ID: 3472384
TEHRAN (IQNA) - Bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari ambalo lilikuwa likiwalenga wakandarasi Uturuki limelipuka katika eneo la Afgoye, kaskazini Magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu ambapo watu watatu wanaripotiwa kuuawa katika tukio hilo.

Duru za usalama zimedokeza kuwa gari hilo ambalo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi liligonga katika eneo ambapo wakandarasi hao wa Uturuki pamoja na maafisa wa polisi walikuwa wakila chakula chao cha mchana.

Haijulikani ni nani aliyetekeleza shambulio hilo lakini wakaazi na maafisa wa polisi wanasema kwamba magaidi wa kundi la al Shabaab walijaribu kushambulia Afgoye, takriban kilomita 30 kutoka Mogadishu, Ijumaa iliopita kabla ya kufurushwa.

Taarifa zinasema vikosi vya jeshi la Somalia vimefanikiwa kuzima shambulizi la usiku wa kuamkia Ijumaa la kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu.

Duru za kijeshi zimearifu kuwa, wanachama wa kundi hilo jana usiku walivamia mji wa Afgoye katika eneo la Lower Shabelle yapata kilomita 30 kusini magharibi mwa Mogadishu, lakini wanajeshi wa serikali walikabiliana nao vikali na kuwarejesha nyuma.

Hata hivyo jeshi la Somalia halijaeleza iwapo kuna askari au mwanamgambo yeyote wa al-Shabaab aliyeuawa katika mapigano hayo ya jana usiku.

Bashir Mayow, mkazi wa mji wa Afgoye amesema milio ya risasi ilirindima masaa kadhaa usiku wa jana wakati wa makabiliano hayo na kusababisha hali ya taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Kundi hilo, linalohusishwa na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda, limekiri kutekeleza mashambulio ya hapo awali katika kampeni zake za kuipindua serikali ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Genge la kigaidi la al Shabab liliundwa mwaka 2007 kwa shabaha ya kuipindua serikali kuu ya Somalia. Mwaka 2011 genge hilo la ukufurishaji lilitimuliwa katika maeneo mengi liliyokuwa linayadhibiti ukiwemo mji mkuu Mogadishu. Hata hivyo bado lina wafuasi wake katika vijiji vya mbali vya Somalia.

3470384

 

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: