Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo asubuhi katika utangulizi wa darsa ya marhala ya juu kabisa ya fiqhi. Ameashiria propaganda kubwa na za sumu za vyombo vya propaganda vya maajinabi za kuwashawishi wananchi wasishiriki katika uchaguzi; na akasema: Propaganda hizo hasi zilianza tangu miezi kadhaa nyuma na zikaongezeka wakati wa kukaribia uchaguzi; na katika siku mbili za mwisho na kwa kisingizio cha kuzuka kirusi na maradhi fulani, vyombo hivyo vya habari havikuacha kutumia kila fursa viliyopata kuwashawishi wananchi wasishiriki katika uchaguzi.
Kiongozi Muadhamu amemshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuwashukuru pia wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi licha ya propaganda chafu zilizofanywa; na akaeleza kwamba: Irada ya Mwenyezi Mungu imelitakia taifa hili lipate ushindi.
Aidha amesema, uadui wa maadui dhidi ya taifa la Iran haukomei katika nyuga za uchumi, utamaduni na imani za kidini na kimapinduzi za wananchi; na akaongezea kwa kusema: Wao wanapinga hata uchaguzi wa taifa la Iran, kwa sababu hawataki ithibitike hakika ya ushiriki wa wananchi katika uchaguzi kwa jina la dini na upigaji kura wao kwa ajili ya Mapinduzi.
Ayatullah Khamenei amesema, kufanyika uchaguzi katika Mfumo wa Kiislamu kunabatilisha madai ya maadui kwamba dini inapingana na uhuru na demokrasia; na akabainisha kuwa: Uchaguzi katika Jamhuri ya Kiislamu unaonyesha kwamba dini ni dhihirisho kamili la demokrasia ya pande zote; na kufanyika chaguzi 37 ndani ya muda wa miaka 41 kunaonyesha umuhimu usio na kifani unaotoa Mfumo wa Kiislamu kwa nafasi ya chaguo la wananchi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa wito kwa wananchi wote wa kuwataka wamtambue adui na kuwa macho katika kukabiliana naye, na akasisitiza kwamba: Katika kukabiliana na harakati za maelfu ya watu wanaotumikia kambi ya adui dhidi ya masuala mbali mbali ya Iran, inapasa wawepo mamilioni ya watu katika kambi ya Iran waliojiandaa kwa ulinzi, kutoa pigo na kujibu mapigo ya mashambulio katika masuala ya uenezi na kazi mbali mbali zinazoweza kufanywa kwa ajili ya taifa.