Rais Rouhani ambaye alikuwa akizungumza mjini Tehran Jumanne katika kikao cha Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Kuzuia Virusi vya Corona, amesema kuwa, taasisi zote hapa nchini zinashirikiana kwa ajili ya kupambana na virusi hivyo na kwamba Iran haina tatizo lolote la kudhamini vipukusi (dawa za kuua vijidudumaradhi), dawa za kijisaffishia mikono na maski.
Rais Rouhani amesema kuwa moja kati ya njama zinazofanywa na maadui ni kuzusha hofu na woga mkubwa katika jamii na kuilemaza nchi na kuongeza kuwa: Katika siku hizi vyombo vya habari vya baadhi ya nchi zinazofanya uhasama dhidi ya Iran vinaeneza mambo yasiyo na ukweli wowote.
Amewataka wananchi wafuate maelekezo ya maafisa wa afya na kubatilisha njama hizo za maadui na kusema siku tatu zijazo mambo yote hapa nchini yatarejea katika hali yake ya kawaida.
Virusi vya Corona viliripotiwa kwa mara ya kwanza Disemba mwaka jana katika mkoa wa Wuhan huko mashariki mwa China. Takwimu zinasema kuwa, virusi hivyo sasa vemeenea katika mikoa 30 ya nchi hiyo na kuvuka mpaka hadi katika makumi ya nchi duniani.
Hadi sasa zaidi ya watu elfu 80 wamepatwa na virusi hivyo katika pembe mbalimbali za dunia. 27 elfu kati yao wametibiwa na kupona virusi hivyo na wengine zaidi ya 2,700 wameaga dunia.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Iran watuu 15 walikuwa wameaga dunia haja jana hapa nchini kutokana na virusi vya Corona na waathirika wengine 95 wanaendelea kupata matibabu.