IQNA

Spika wa Bunge la Iran
13:24 - March 05, 2020
News ID: 3472534
TEHRAN (IQNA)- Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameeleza kusikitishwa kwake na mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu nchini India na ameitaka serikali ya New Delhi, itumie mbinu na uwezo wote kwa ajili ya kuhitimisha mzozo uliopo kwa njia za amani.

Ali Larijani amesema hayo leo na kueleza kwamba, Waislamu ni sehemu ya utamaduni na jamii ya India ambao walikuwa na nafasi muhimu katika kuleta ustawi na maendeleo ya nchi hiyo.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taswira na kinachofahamika kutoka katika sheria mpya inayojulikana kama haki ya uraia nchini India kinabainisha kubanwa Waislamu na hili ndilo jambo lililozusha wasiwasi.

Amesisitiza kuwa, India ni ardhi ya kaumu, lugha, dini na tamaduni mbalimbali hivyo kuibuka mambo kama hayo ni jambo linalokinzana wazi na moyo wa utamaduni na ustaarabu wa Kihindi.

Spika Larijani amekumbushia umuhimu wa uhusiano wa Tehran na New Delhi na kueleza kuwa, kuimarishwa mazungumzo na utamaduni wa kuishi kwa amani baina ya kaumu na dini mbalimbali nchini India ni jambo la dharura.

Sheria mpya ya uraia nchini India inaruhusu kupewa uraia wahajiri wasio Waislamu waliokimbilia nchini humo kutoka nchi jirani za Bangladesh, Pakistan na Afghanistan, huku ikiwanyima haki hiyo ya uraia Waislamu.

Sheria hiyo imepingwa na jamii ya Waislamu nchini humo, asasi za kiraia na hata baadhi ya wanachama waandamizi wa chama tawala nchini humo cha Bharatiya Janata (JBP) ambao wanasema kuwa, sheria hiyo ni ya kibaguzi.

3883409

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: