IQNA

Baadhi ya misikiti yafunguliwa Senegal

19:49 - May 16, 2020
Habari ID: 3472772
TEHRAN (IQNA) – Rais Macky Sall wa Senegal ameidhinisha baadhi ya misikiti kuanza kuswaliwa jamaa katika nchi hiyo kwa sharti la kuzingatiwa kanuni za kiafya za kukabiliana na COVID-19.

Kwa mujibu wa taarifa, siku ya Ijumaa maelfu ya waumini walimiminika katika Msikiti wa Massalikul Jinaan, ulio katika mji mkuu Dakar na ambao ni kati ya misikiti mikubwa zaidi Afrika Magharibi ambao unasimamiwa na Tariqa ya Mouride.

Msemaji wa msikiti huo Mor Daga Syllah amesema maafisa wa kidini wamewataka waumini wanaofika msikitini hapo kutumia sanitaiza kuosha mikono na kukaa umbali wa mita moja kila moja.

Katika eneo la Mbao, nje kidogo ya mji wa Dakar waumini pia walionekana wakitumia sabuni kunawa mikono huku aghalabu wakiwa wamevaa barakoa.

Hadi sasa watu 2,310 wa Senegal wameambukizwa corona na 25 wamefariki.

Senegal bado imefunga shule na mipaka na kuna vizingiti katika usafiri huku sheria ya kutotoka nje usiku ikitekelezwa kuzuia kuenea COVID-19.

3471431

captcha