IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Vita dhidi ya Afghanistan, Iraq na Syria ni miongoni mwa sababu za kuchukiwa Marekani

12:08 - May 18, 2020
Habari ID: 3472777
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, kuwasha moto wa vita katika nchi kadhaa ikiwemo Afghanistan, Iraq na Syria ni miongoni mwa sababu za kuchukiwa Marekani na akabainisha kwamba, Wamarekani wanaeleza kinagaubaga kuwa 'tumeweka vikosi Syria kwa sababu kuna mafuta'; lakini bila shaka hawataweza kubaki, si Iraq wala Syria. Ni lazima waondoke huko na hakuna shaka kuwa wataondoshwa tu.

Ayatullah Khamenei aliyasema hayo jana jioni katika kikao alichofanya kwa njia ya video na hadhara ya vijana wanachuo pamoja na jumuiya za vyuo vikuu nchini.

Katika hotuba yake kwa wanachuo hao, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema, kuchomwa moto bendera ya Marekani katika nchi nyingi duniani na hata ndani ya Marekani kwenyewe ni ithibati mojawapo ya chuki yalizonazo mataifa kwa utawala huo na akaongeza kuwa: Mbali na mataifa, hata maraisi wa baadhi ya nchi washirika wa Marekani pia, wakati wanapoeleza yaliyomo nyoyoni mwao wanadhihirisha chuki zao kwa viongozi na utawala wa Marekani na wala hawauamini wala kuujali utawala huo.

Ayatullah Khamenei amesema, chuki za hivi sasa dhidi ya Marekani, kwa sehemu moja zinatokana na tabia ya viongozi wake wa sasa akiwemo rais na waziri wa mambo ya nje wa utawala huo ambao ni watu wasio na thamani, wanaozungumza upumbavu, waropokaji na wasio na mantiki na akaongeza kwamba, bila shaka si suala hilo tu linalosababisha chuki dhidi ya Marekani, lakini chuki hizo zinatokana pia na utendaji wa muda mrefu wa Marekani ukiwemo wa kufanya mauaji, jinai, uonevu, kuanzisha ugaidi, kuzisaidia tawala za kidikteta na zinazosifika kwa ubaya, kuunga mkono bila kusitasita dhulma zinazoongezeka kufanywa kila leo na utawala wa Kizayuni na hivi karibuni kabisa ni utendaji wake wa kufedhehesha katika kadhia ya corona.

Katika kikao hicho na wanachuo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia kusimama imara Iran na kwa nguvu kamili katika kukabiliana na utumiaji mabavu na pia uwezo imara wa kitaifa unaoshuhudiwa hivi sasa; na akaeleza kwamba, pamoja na hayo nukta ya kuzingatia ni kuwa, adui hajakata tamaa kuhusu njama yake ya kutaka kulidunisha taifa na kudhoofisha moyo wa kujiamini kitaifa; lakini licha ya yote anayofanya adui, Mwenyezi Mungu amekadiria kinyume chake katika takdiri yake.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, hata katika kadhia zinazohusiana na corona ikiwemo namna ugonjwa huo ulivyoshughulikiwa nchini ikilinganishwa na Magharibi, jitihada za kielimu zilizofanywa kwa ajili ya kukitambua kirusi hicho, harakati kubwa ya kutoa misaada kwa watu kiimani na vile vile utumaji wa satalaiti angani vimejenga hisia za kuwa na izza na nguvu kubwa zaidi kwa taifa la Iran.

3471456

captcha