IQNA

15:46 - June 03, 2020
News ID: 3472830
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema yanayojiri siku hizi Marekani yameweka wazi ukweli uliokuwa umefichwa nchini humo kuongeza kuwa: "Wamarekani wamefedheheka duniani kutokana na mienendo yao."

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumatano katika hotuba ya moja kwa moja kwa njia ya televisheni kwa mnasaba wa kukumbuka kuagadunia Imam Khomeini (MA) muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: "Si jambo jipya kumuona afisa wa polisi wa Marekani akimkanyaga mtu mweusi na kumfinya shingo kwa goti hadi kufa huku kitendo hicho kikishuhudiwa na maafisa wengine wa polisi." Ameongeza kuwa,  jinai sawa na hii imeshuhudiwa ikitendwa na utawala wa Marekani katika nchi zingine kama vile Afghanistan, Iraq, Syria na Iraq.

Ayatullah Khamenei amesema nara na kauli mbiu ya Wamarekani  hii leo ambayo ni 'hatuwezi kupumua' ni kauli ya kwanza ya mataifa yote yanayodhulumiwa na kuongeza kuwa: "Marekani imefedheheka kutokana na mienendo yake. Ugonjwa wa corona uliibuka Marekani baada ya kuenea katika nchi zingine, kwa hivyo walikuwa na uwezo wa kutumia uzoefu wa nchi zingine na wangeweza kujitayarisha lakini wameonyesha udhaifu na wameshindwa kukabiliana na corona kutokana na ufisadi katika serikali yao." Kiongozi Muadhamu ameendelea kusema kuwa: "Katika kukabiliana na watu wake, Marekani imeonyesha utendaji mbovu zaidi. Wanaua watu na kudai eti wao ni watetezi wa haki za binadamu. Kwani huyo mtu mweusi mliyemuua si mwanaadamu."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hisia ya Wamarekani kuhisi kuaibika kutokana na utendaji wa serikali yao na watawala wa sasa wa nchi hiyo na kusema: "Kutokana na hali iliyojitokeza idadi kubwa ya watu ambao kazi yao ni kuitetea Marekani na kuikuza sasa hawawezi tena kunyanyua vichwa vyao."
Ayatullah Khamenei katika sehemu nyingine ya hotuba yake amesema: "Kutaka Mabadiliko, Kuwa na Motisa wa Kuleta Mabadiliko na Kuibua Mabadiliko" ni kati ya sifa muhimu zaidi za Imam Khomeini (MA) na kuongeza kuwa wakati wa mwanzo wa muamko wa Kiislamu wengi hawakuwa na ufahamu wa mustakabali lakini Imam Khomeini (MA) aliweza kutazama mustakabali na kudiriki  yanayojiri sasa katika taifa yaani kuundwa Umma wa Kiislamu na kuibua utamaduni mpya wa Kiislamu katika mustakabali." 
Kiongozi Muadhamu ameendelea kwa kubainisha matokeo muhimu sana ya mabadiliko kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA), kusimama kidete na kiyafedhehesa madola makubwa na kuongeza kuwa: "Kuna wakati ambao mtu hangaweza kudhani kuwa inawezekana kukabiliana na Marekani lakini Imam Khomeini alilieta mabadiliko katika mtazamo wa watu kuhusu madola makubwa. Aliweza kuyadhalilisha madola makubwa na kuthibitisha kuwa, wanaotumia mabavu duniani wanaweza kupata pigo na ukweli huu uliweza kushuhudiwa katika kusambaratika Shirikisho la Sovieti na yanayojiri leo Marekani." 

/3902839

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: