IQNA

21:43 - June 26, 2020
News ID: 3472899
TEHRAN (IQNA) - Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limetangaza kuwa, idadi ya watoto wanaosumbuliwa na utapiamlo imeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini Yemen.

Ripoti iliyotolea na UNICEF imeashiria kwamba kiwango kikubwa cha watoto wa Yemen wenye umri wa chini ya miaka mitano wanaosumbuliwa na utapiamlo kimefikia asilimia 20 ambayo sawa na nusu ya watoto wote wa Yemen na kuongeza kuwa, hali mbaya zaidi ya utapiamlo baina ya watoto inashuhudiwa katika mikoa ya al Hudaydah, Sa'dah, Taiz na Lahij.

UNICEF imesema kuwa maradhi ya kipindupindu ni miongoni mwa mambo yanayohatarisha uhai wa watoto wa Yemen.

Hali ya afya ya Wayemeni inatajwa kuwa mbaya sana kutokana na vita na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake kwa zaidi ya miaka 5 dhidi ya taifa hilo.

Mwaka 2017 Umoja wa Mataifa uliiweka Saudi Arabia katika orodha nyeusi ya wauaji na wakiukaji wakubwa wa haki za watoto kutokana na mauaji ya maelfu ya watoto wa Yemen na kuharibiwa shule na mahospitali ya nchi hiyo katika mashambulizi ya Saudia.

Hata hivyo siku chache zilizopita Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliliondoa jina la Saudi Arabia katika orodha hiyo. Mashirika mbalimbali ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kama vile Amnesty International, Human Rights Watch na Save the Children yamemjia juu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kukosoa vikali uamuzi wake huo.

Guterres amefanya uamuzi huo ikiwa ni chini ya wiki moja baada ya Kituo cha Haki za Binadamu cha Ainul Insaniya kutoa ripoti na kutangaza kuwa, tokea muungano wa Saudia uanzishe vita dhidi ya Yemen mnamo Machi 26, 2015 hadi sasa, watu 16, 672 wamepoteza maisha na miongoni mwao kuna watoto 3,742 na wanawake 2,364.

3906955

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: