IQNA

UN yakosolewa kwa kuiondoa Saudia katika orodha ya wanaokiuka haki za watoto

20:23 - June 16, 2020
Habari ID: 3472870
TEHRAN (IQNA)- Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamemjia juu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kwa kuuondoa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika orodha ya makundi yanayokanyaga haki za watoto.

Ripoti mpya ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, muungano huo wa kijeshi wa Saudia utaondolewa katika orodha ya makundi yanayoua na kukiuka haki za watoto, kutokana na kupungua madhara dhidi ya watoto katika mashambulizi yake ya anga.

Human Rights Watch imemkosoa vikali Guterres kwa kuundoa muungano huo wa kijeshi wa Saudia katika 'orodha ya fedheha' ikisisitiza kuwa, amepuuza ushahidi wa Umoja wa Mataifa wenyewe, unaoonyesha kuendelea kukanyagwa haki za watoto wa Yemen.

Naye afisa wa shirika la Save the Children, Inger Ashing ameeleza juu ya kusikitishwa kwake na 'uamuzi huo wa kutisha' wa Umoja wa Mataifa akisisitiza kuwa umechukuliwa kutokana na mashinikizo.

Kadhalika shirika la kutetea haki za watoto katika migogoro ya kivita (Watchlist on Children and Armed Conflict) limesema kwa kutoubebesha dhima muungano huo vamizi wa Saudia na Imarati, Katibu Mkuu wa UN amewaweka watoto wa Yemen katika hatari zaidi ya kuendelea kushambuliwa. 

Wakati huo huo, Harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah imeutaka Umoja wa Mataifa kutupilia mbali uamuzi wake wa kuliondoa jina la Saudi Arabia na washirika wake katika orodha ya makundi yanayokanyaga na kuvunja haki za watoto.

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Watu wa Yemen, Muhammad Ali al Houthi ameashiria jinai na uhalifu unaoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen na kusema kuwa, hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuliondoa jina la Saudia katika orodha ya makundi yanayokanyaga haki za watoto ni jinai na inaakisi kupuuzwa vigezo vya kibinadamu. 

Al Houthi ameongeza kuwa, Umoja wa Mataifa umetangaza habari hiyo sambamba na mashambulizi makali ya Saudi Arabia na washirika wake katika mkoa wa Saada huko kaskazini mwa Yemen ambayo yameua raia 12 wakiwemo wanawake na watoto wadogo kadhaa.

Guterres amefanya uamuzi huo ikiwa ni chini ya wiki moja baada ya Kituo cha Haki za Binadamu cha Ainul Insaniya kutoa ripoti na kutangaza kuwa, tokea muungano wa Saudia uanzishe vita dhidi ya Yemen mnamo Machi 26, 2015 hadi sasa, watu 16, 672 wamepoteza maisha na miongoni mwao kuna watoto 3,742 na wanawake 2,364.

Wiki iliyopita, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen alisema kuwa, Umoja wa Mataifa ni mhusika wa jinai za muungano vamizi wa Saudia dhidi ya taifa hilo maskini la Kiarabu.

3471718

captcha