IQNA

Wabunge Tunisia wapanga kumuondoa Spika Rached Ghannouchi

13:05 - July 13, 2020
Habari ID: 3472959
TEHRAN (IQNA) – Vyama vitano vya kisiasa nchini Tunisia vimezindua mpango wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na spika wa bunge la nchi hiyo Rached Ghannouchi ambaye anatuhimiwa kupembelea upande mmoja.

Hayo yanajiri wakati chama chake cha Ennahda kimetaka serikali mpya iundwe kutokana na kuendelea mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Kura ya kutokuwa na imani na Ghannouchi ni changamoto kubwa zaidi kwa chama cha Ennahda, ambacho kiliingia madarakani kufuatia mwamko wa Kiislamu wa Februari mwaka 2011 nchini humo ambao ulipelekea kuangushwa utawala wa kidikteta nchini humo. Katika uchaguzi uliofuata chama cha Ennahda kiliweza kuunda serikali baada ya kupata asilimia 37 kura katika uchaguzi wa Oktoba 2011. Hatahivyo chama hicho kililazimika kuondoka madarakani mwaka 2014 kufuatia maandamano ya wananchi.

Serikali ya Tunisia inashinikizwa kujiuzulu baada ya wapinzani kudai kuwa Waziri Mkuu Elyes Fakhfakh hastahiki kuwatawala kutokana na kashfa za ufisadi. Ennahda, ambacho ni chama kikuu katika serikali ya mseto kinasema kinaunga mkono mabadiliko ya serikali.

Jaji mmoja ameanzisha uchunguzi kuhusu madai dhidi ya Fakhfakh na kwamba waziri wa kupambana na ufisadi naye ameunda timu maalumu ya kuchunguza madai hayo na kuitaka iwasilishe ripoti yake kwake katika kipindi cha wiki tatu zijazo.

Tume ya taifa ya kupambana na ufisadi nchini Tunisia nayo imesema kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo hakuieleza tume hiyo kwamba makampuni ambayo ana hisa ndani yake, yana mikataba na serikali.

Katika upande mwingine, vyama vya Tahya Tounes, Attayar, Chaab na Mageuzi ambavyo viko katika muungano na Ennahda vinasema Spika Ghannouchi anatumikia ajenda ya Harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin ya Misri, harakati ambayo inasemekana kuwa na mfungamano na Qatar pamoja na Uturuki. Ghannouchi amekanusha tuhuma hizo huku akisisitiza kuwa Watunisia wanataka serikali yenye kuzingatia masuala ya kiuchumi na kijamii na si malumbano ya kisiasa.

3471984

Kishikizo: Tunisia ، Ennahda
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha