IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Uchumi wa Iran usifungamanishwe na matukio ya kigeni, Marekani ni mfano wa wazi wa kushindwa

16:32 - August 23, 2020
Habari ID: 3473096
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, mipango ya uchumi kwa ajili ya nchi haipaswi kusimama na kusubiria kuondolewa vikwazo au matokeo ya uchaguzi wa nchi fulani na kusisitiza kwamba, uchumi wa nchi kwa namna yoyote ile haupaswi kufungamanishwa na matukio ya nje kwani hilo ni kosa la kistratejia.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo leo kwa mnasaba wa Wiki ya Serikali wakati alipofanya kikao kwa njia ya mawasiliano ya intaneti na Rais Hassan Rouhan pamoja na baraza lake mawaziri na kueleza kwamba, inapaswa kujaalia kwamba, vikwazo vitaendelea kwa muda wa miaka kumi ijayo na kwa msingi huo kuna haja ya kuzingatia na kujikita katika kutumia suhula na nyenzo za ndani na masuala ya kiuchumi hayapaswi kufungamanishwa na matukio ya nje.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewahutubu viongozi na maafisa wote wa serikali kwa kusema: Utumishi katika mfumo wa Kiislamu una thamani maradufu ambapo mnapaswa kulitahamni hili, kwani kutoa huduma katika Jamhuri ya Kiisamu kunasaidia kuonyesha na kudhihirisha kigezo cha Uislamu kwa ajili ya kujenga jamii na usimamizi wa jamii na ndio maana jambo hili lina umuhimu maradufu.

Ayatullah Khamenei ameashiria kushindwa maktaba mbalimbali za kifikra za mwanadamu kwa ajili ya kuiongoza jamii na kuitaja Marekani kama mfano wa wazi wa kushindwa na kuongeza kuwa, thamani za mwanadamu kama uzima, uadilifu na usalama ni mambo ambayo yamekuwa yakikanyagwa na kukiukwa nchini Marekani kuliko sehemu nyingine yoyote ya dunia.

Ameongeza kuwa, mbali na matatizo ya ndani na ya uongozi, masuala kama kuanzisha vita, kufanya mauaji na kuvuruga usalama ni miongoni mwa kazi za leo za Marekani ambazo zimeenea huko Syria, Palestina, Yemen na kabla ya hapo katika nchi kama Iraq, Afghanistan na maeneo mengine kama Vietnam na Hiroshima.

3918385

captcha