IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Tunalaani mwenendo wa ubaguzi wa rangi wa Marekani na tunaunga mkono harakati ya wananchi

19:31 - July 29, 2020
Habari ID: 3473011
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Katika matukio ya sasa ya Marekani na harakati ya kupinga ubaguzi wa rangi iliyopo, msimamo wetu thabiti ni wa kuwaunga mkono wananchi na kulaani mwenendo wa kikatili wa utawala wa ubaguzi wa rangi wa nchi hiyo."

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ameyasema hayo katika ujumbe kwa mnasaba wa masiku ya Hija na akabainisha kuwa: Kuyaangalia yanayojiri katika barabara za Marekani, mwenendo wa viongozi wa Marekani kwa wananchi wao, mpasuko mkubwa wa tofauti za kitabaka ndani ya nchi hiyo, udhalili na upumbavu wa watu waliochaguliwa kuongoza nchi hiyo, ubaguzi wa rangi wa kutisha ulioko huko pamoja na ukatili wa askari wake ambaye anaweza kwa utulivu, tena mbele ya macho ya wapita njia kumtesa na kumuua barabarani mtu asiye na hatia yoyote, kunaweka wazi kabisa upeo wa hali mbaya sana ya kiakhlaqi na kijamii ya ustaarabu wa Magharibi na upotofu na ubatilifu wa falsafa yake ya kisiasa na kiuchumi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Muamala wa Marekani kwa mataifa dhaifu ni taswira pana ya mwenendo wa yule askari polisi aliyemwekea goti la shingo mtu mweusi asiyeweza kujihami na akambinya mpaka akafika hadi ya kukata roho.

Ayatullah Khamenei ameielezea Hija kuwa ni mazoezi ya kujipima nguvu na uwezo wa kukabiliana na waistikbari, ambao ni kitovu cha ufisadi, dhulma, uuaji wa wanyonge na uporaji; na kwamba leo hii kiwiliwili na roho ya umma wa Kiislamu vinahujumiwa na kutapakaa damu kwa udhalimu na ukhabitihi wa waistikbari hao; na akasisitiza kwamba: "Tunavyoamini, kuwepo Marekani Asia Magharibi ni kwa madhara ya mataifa ya eneo hili na kunazisababishia nchi uharibifu, kubaki nyuma kimaendeleo na kukosa amani."

Sambamba na kutilia mkazo umoja wa umma wa Kiislamu katika kukabiliana na Marekani mvamizi pamoja na utawala wa Kizayuni, na vilevile ulazima wa kufanya hima ya "kuisaidia Palestina inayodhulumiwa, kukihurumia kiwiliwili kilichojeruhiwa cha taifa la Yemen na kuwashughulikia Waislamu wanaodhulumiwa katika kila pembe ya dunia", Ayatullah Khamenei amewanasihi viongozi wa baadhi ya nchi za Kiislamu, - ambao badala ya kutegemea ndugu zao Waislamu, wanakimbilia na kujikumbatisha kwa adui, na kwa sababu ya manufaa binafsi ya siku chache wanavumilia kuburuzwa na kudhalilishwa na adui huyo na kuwa tayari kuipiga mnada heshima na uhuru wa mataifa yao,- waache tabia hiyo ya kujidhalilisha.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia maendeleo iliyopta Iran ya Kiislamu na akabainisha kwamba, "shetani mkubwa zaidi haramia na haini wa zama hizi yaani utawala wa Marekani ameshindwa kututisha au kutushinda kwa hila na ghilba yake au kuzuia maendeleo yetu ya kimaada na kimaanawi".

3913419

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha