IQNA

Israel yaendeleza hujuma dhidi ya Ghaza, yawaua Wapalestina wanne

17:30 - August 25, 2020
Habari ID: 3473100
TEHRAN (IQNA)- Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendeleza hujuma zake dhidi ya Ukanda wa Ghaza kwa kuwaua shahidi Wapalestina wanne.

Kwa mujibu wa taarifa, Wapalestina hao wameuawa shahidi baada ya ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia kwa mabomu maeneo kadhaa ya Palestina huko mashariki mwa Ukanda wa Ghaza.

Raia hao wa Palestina katika eneo la Ghaza, ambalo liko chini ya mzingiro wa kinyama wa Israel, waliuawa katika hujuma hiyo ya anga ya jeshi katili la Israel jana Jumatatu na wametambuliwa kama Iyad Jamal al-Jidi, Muataz Amir al-Mubid, Yahya Fareed al-Mubid na Yaaqoub Zaydieh.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema "wanne hao wameuawa katika mripuko uliotokea wakiwa katika jitihada za kuwaondoa watenda jinai katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu."

Habari zaidi zinasema kuwa, Wapalestina hao wameuawa shahidi wakiwa katika kambi ya kijeshi ya harakati ya Jihadul Islami, katika mji wa Shejaiya, mashariki mwa Gaza.

Hata hivyo utawala haramu wa Israel unadai kuwa haujahusika na shambulizi hilo la anga, na eti vijana hao wa Kipalestina wameaga dunia baada ya kuripukiwa na bomu walilokuwa wakiliunda.

Eneo la Ukanda wa Ghaza mbali na kushuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya jeshi katili la Israel, kwa zaidi ya miaka 14 sasa limekuwa chini ya mzingiro wa anga, baharini na nchi kavu unaotekelezwa na utawala ghasibu wa Israel.

/3472370

captcha