IQNA

18:18 - September 22, 2020
Habari ID: 3473194
TEHRAN (IQNA) – Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeupa utawala haramu wa Israel muhula mwa miezi miwili kuhitimisha mzingiro wake wa miaka 12 dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Khalil al-Hayya, afisa mwandamizi katika Idara ya Kisiasa ya Hamas, amesema Israel inazuia misaada ya kibinadamu kuingia Ghaza hata wakati huu wa janga la corona.

Al Hayya amesema iwapo Israel haitasitisha mzingiro, basi ifahamu kuwa Hamas inauwezo wa kijeshi wa kuwalazimu Waisraeli walazimike kwenda kuishi kwenye maficho kutokana na mashambulizi.

Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa Katika Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati Nickolay Mladenov alitembelea Ghaza Septemba 16 na kufanya mazungumzo na maafisa wa Hamas kuhusu mzingiro dhidi ya eneo hilo.

Kiongozi wa Hamas Ismail Haniya amesema harakati hiyo na watu wa Ghaza wako tayari kukabiliana na mzingiro huo wa kidhalimu hadi uondolewe. Hamas imekataa msaada wa dola bilioni 15 ambao sharti lake lilikuwa ni kuweka chini silaha. Haniya amesema msaada huo ulikuwa umetolewa katika fremu ya mpango wa rais Donald Trump wa Marekani wa kuupa nguvu utawala haramu wa Israel na kuwadhoofisha Wapalestina.

Mpango huo wa Trump uliopewa jina la 'muamala wa karne', ulikataliwa tangu mwanzoni na Wapalestina wakiungwa mkono na jamii ya kimataifa na mataifa jirani ya eneo la Asia Magharibi,  ulimwengu wa Kiislamu na hata idadi kubwa ya wajumbe wa chama cha upinzani cha Democrat katika Bunge la Kongresi la Marekani.

Tarehe 28 Januari, rais Donald Trump wa Marekani akiwa pamoja na waziri mkuu wa utawala bandia wa Israel, Benjamin Netanyahu alizindua mpango wa ubaguzi wa kimbari wa Muamala wa Karne.

Kuitambua rasmi Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, kuupatia utawala huo haramu umiliki wa asilimia 30 ya eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, kupingwa haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea nchini kwao na kupokonywa silaha kikamilifu ile itakayoitwa nchi ya Palestina ni miongoni mwa vipengele vya mpango huo wa udhalilishaji.

Tokea mwaka 2006, utawala wa Kizayuni wa Israel uliweka mzingiro wa nchi kavu, anga na baharini dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza. Katika mzingiro huo, Israel inazuia bidhaa muhimu kama vile, petroli, umeme, dawa, chakula na vifaa vya ujenzi kufika katika Ukanda wa Ghaza.

3472613

Kishikizo: ghaza ، mzingiro ، palestina ، hamas ، Israel
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: