Kwa mujibu wa taarifa, kamati ya tuzo ya amani ya Nobel yenye makao yake nchini Norway leo imelitangaza Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP kuwa ndio mshini wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huuu wa 2020.
Ikitangaza tuzo hiyo kamati imesema “ni kwa sababu ya mchango mkubwa wa WFP katika kupambana na njaa, kwa mchango wake wa kuleta mazingira ya amani katika maeneo yenye migogoro na kwa kuwa chachu ya juhudi za kuzuia njaa kutumika kama silaha ya vita na migogoro.”
Kwa upande wake WFP ikishukuru kwa tuzo hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter imesema “Hii ni kutambua kazi kubwa ya wafanyakazi wa WFP ambao wanaweka Maisha yao hatarini kila siku ili kufikisha chakula na msaada kwa zaidi ya watu milioni 100 wenye njaa wakiwemo Watoto, wanawake na wanaume kote duniani.”
Akiipongeza WFP kwa ushindi huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Nimefurahi kwa uamuzi wa kamati ya tuzo ya amani ya Nobel kulitunukia shirika la Umoja wa Mataifa la WFP tuzo ya amani yam waka huu. WFP ndilo shirika la kwanza duniani kuwa msitari wa mbele kukabiliana na kutokuwa na uhakika wa chakula. Waume na wanawake wa WFP wanawanapitia hatari na safari ndefu kufikisha msaada wa kuokoa Maisha kwa wale walioathirika na migogoro, kwa watu wanaotaabika sababu ya majanga, kwa Watoto na familia wasio na uhakika mlo wao unaofuta unatoka wapi.”
Tuzo hiyo, ambayo huwa medali ya dhahabu na cheki ya Krona milioni 10 za Sweden sawa na dola milioni 1.1 za Marekani, itakabidhiwa rasmi tarehe 10 Disemba, siku ya kumbukumbu ya kifo cha mwasisi wa tuzo hiyo, Alfred Nobel (1833-1896).