Vitisho na hotuba za chuki dhidi ya Waislamu wa Australia vimeongezeka ambapo katika tukio la karibuni, msikiti mmoja ukipokea simu za matusi kwa makumi huku kukiwa na taarifa za watu kushambuliwa mitaani. Wakati jamii ya Kiyahudi ikikabiliana na majonzi ya shambulio lililoua watu 15 katika hafla ya Hanukah, viongozi wa dini wanasema mgawanyiko wa kijamii na kisiasa umepelekea makundi mengine kushambuliwa kwa chuki.
Islamophobia Register Australia ilipokea ripoti 126 za matukio ya chuki katika wiki moja baada ya mauaji ya risasi ya tarehe 14 Disemba – mara kumi zaidi ya ilivyopokea katika wiki mbili zilizotangulia. Baraza la Maimamu wa Australia pia limesajili ongezeko la matukio. Makamu wa rais wake, Ahmed Abdo, alisema wanawake Waislamu wamekosolewa kwa maneno ya matusi na hata kuonyeshwa ishara za mikono zinazofanana na bunduki. “Kuna hofu kubwa,” alisema Abdo. “Mwanamke mmoja hataki kutoka nyumbani kwa sababu anavaa hijabu, na anaogopa kushambuliwa. Kuna hisia kwamba huenda ukatokea unyanyasaji wa chuki dhidi ya Waislamu.”
Polisi wamesema shambulio la Bondi lilihusishwa na Daesh (ISIL/ISIS). Viongozi na mashirika ya Kiislamu wamelaani shambulio hilo, na wawakilishi wao walihudhuria dua na kumbukumbu za waliouawa. Hata hivyo, siku moja baada ya shambulio, vichwa vya nguruwe vilivyokatwa na sehemu za wanyama ziliwekwa katika lango la makaburi ya Kiislamu kusini-magharibi mwa Sydney. Msikiti mmoja wa Queensland na shule ya Kiislamu huko Victoria pia viliharibiwa kwa maandiko ya matusi wiki hiyo. Mitandaoni, kulisambazwa wito wa “kupiga Mashariki ya Kati” katika ufukwe wa Cronulla, na mtu mmoja ameshtakiwa kwa hilo.
Abdo alisema baadhi ya waumini Sydney wamepunguza muda wa kukaa msikitini, wakiondoka mara tu baada ya sala. Msikiti wa Lakemba umeongeza ulinzi wake. Mohamed Mohideen, rais wa Baraza la Kiislamu la Victoria (ICV), alisema kituo cha sala cha shirika hilo kimekumbwa na barua pepe za chuki kwa wingi na yeye binafsi amepokea simu za vitisho zaidi ya 30. “Huonekana mtandaoni, ingawa ni chuki, au hujitokeza kwa matusi, na huenda pia ikafikia madhara ya kimwili,” alisema Mohideen.
ICV imeripoti vijana wa kike waliovaa hijabu na waumini nje ya misikiti kutukanwa tangu tarehe 14 Disemba, jambo lililosababisha doria zaidi za polisi. “Tunao hofu mtu anaweza kufanya jambo lolote wakati wowote … lakini jamii ya Kiislamu ni imara. Hatutadai kuwa wahanga, hatutajificha.” Mohideen alisema mjadala wa kisiasa kuhusu “Uislamu mkali” baada ya shambulio la Bondi umeongeza uhasama dhidi ya Waislamu. “Jamii ya Kiyahudi haikutushambulia … bali ni wanasiasa,” alisema.
Jumanne, waziri mkuu wa New South Wales, Chris Minns, alitembelea msikiti wa Masjid Al-Hidayah Rockdale pamoja na David Ossip, rais wa Baraza la Kiyahudi la NSW.
Msikiti huo ulikuwa umeheshimu kumbukumbu ya waliouawa 15 Jumapili. Minns alikanusha lugha yake kuchochea mgawanyiko, akisema iwapo mtu atashambulia au kudhalilisha familia ya Kiislamu, kiongozi wa Kiislamu au mwanamke Mwislamu, polisi “wameonyesha kuwa watakabiliana na misimamo mikali au ubaguzi bila kujali ni nani anayehusika.”
Katibu wa msikiti, Jashim Uddin, alisema kwa kuwasha menorah “tunataka kupunguza mvutano katika jamii.” Aliongeza: “Tunataka kuonyesha kuwa sote tuko pamoja, siyo tofauti. Si Mwislamu au Myahudi au Mkristo … hatupaswi kulaumiana.”
Hayo yanajiri wakati ambao Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese hivi karibunu ametembelea Hospitali ya St. George kusini mwa Sydney ili kumjulia hali Ahmed Al Ahmed, Mwislamu aliyehatarisha maisha yake kwa kumvamia na kumpokonya bunduki mmoja wa wahusika wa shambulio lililotokea kwenye Ufukwe wa Bondi na kusababisha vifo vya watu 15.Akiwa amesimama kando ya kitanda cha hospitali alicholazwa Al Ahmed, Albanese amemsifu baba huyo wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 43 kwa ujasiri wake wa ajabu, akimtaja kama nembo ya umoja wa kitaifa katika kukabiliana na ugaidi.Katika ujumbe alioweka baadaye kwenye mtandao wa kijamii wa X, Waziri Mkuu wa Australia amemhutubu Muislamu huyo: "Ahmed, wewe ni shujaa wa Australia. Ulijitia hatarini kuwaokoa wengine, ukaikimbilia hatari kwenye Ufukwe wa Bondi na kumpokonya silaha gaidi. Katika nyakati mbaya zaidi, tunawaona Waaustralia walio bora kabisa.
Na hivyo ndivyo tulivyoona Jumapili usiku".Albanese amemalizia ujumbe wake kwa kusema: "kwa niaba ya kila Muaustralia, nasema ahsante".Al Ahmed alijeruhiwa vibaya baada ya kumvamia mmoja wa washambuliaji, akimnyang'anya silaha yake na kumgeuzia, na kumlazimisha mshambuliaji huyo kujisalimisha. Al Ahmed alifyatuliwa risasi mara kadhaa na kupata majeraha kwenye mkono na bega lake. Hata hivyo maafisa wa hospitali wamesema hali yake si mbaya.
3495834