IQNA

Utawala wa Israel walazimika kumuachilia huru Maher al Akhras

20:17 - November 26, 2020
Habari ID: 3473395
TEHRAN (IQNA) - Utawala dhalimu wa Israel hatimaye umelazimika kumuachilia huru Maher al Akhras mateka wa Kipalestina ambaye alikabiliana pakubwa na utawala huo.

Maher al Akhras leo Alhamisi amewasili katika Ukingo wa Magharibi baada ya kuachiwa kutoka jela na inatazamiwa kwamba  atafikishwa kwanza katika hospitali ya al Najah katika mji wa Nablus kwa ajili ya matibabu. 

Maher al Akhras mwenye umri wa miaka 49 mkazi wa kitongoji cha  Silah Adh-Dhuhr huko Jenin aligoma kula chakula kwa karibu siku 103 akilalamikia hukumu ya kutiwa kwake mbaroni pamoja na mateka wengine wa Kipalestina. Katika muda huo wote, mahakama za utawala wa Kizayuni zilipinga kumuachia huru al Akhras licha ya hali yake ya kiafya kuwa mbaya na taasisi za kimataifa na za kisheria kutaka kusitishwa siasa za utawala huo za kukamata na kuwafunga Wapalestina kiholela.

Makundi ya muqawama ya Palestina pia mara kadhaa yaliwatahadharisha viongozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni kuhusu hali mbaya ya kiafya ya Maher al Akhras na taathira zake hasi. 

Mfungwa huyo Mpalestina kwa mara nyingine tena ameweka wazi msimamo wake unaopinga suala la utiwaji mbaroni kiholela raia wa Palestina kunakofanywa na utawala wa Kizayuni jambo lililompelekea achukue hatua ya kugoma kula kwa muda mrefu.  Karibu  mateka wa Kipalestina 4,800 wanashikiliwa katika jela mbalimbali za utawala wa Kizayuni. 

3937521

 

captcha