IQNA

Aplikesheni nyingine ya Swala yaiuzia Marekani taarifa za Waislamu

19:55 - January 12, 2021
Habari ID: 3473549
TEHRAN (IQNA) – Aplikesheni mashuhuri ya simu za mkononi ambayo Waislamu huitumia kubaini wakati wa swala imekuwa ikikusanya kwa siri taarifa za watumizi na kuzikabidhi Marekani.

Kwa mujibu wa  Jarida la Vice, mtandao wa madalali wa data umeuganisha aplikesheni hiyo na taasisi za kiusalama za Marekani kama vile ICE na FBI. ICE ni Kikosi Maalumu cha  Mamlaka ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani nayo FBI ni  Idara ya Upelelezi ya Marekani ambayo kimsingi ni taasisi kuu ya ujasusi na usalama wa ndani nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa aplikeshni hiyo ambayo inajulikana kama Salaat First iliundwa ili kuwasaidia Waislamu kutekeleza faradhi ya swala za kila siku ambapo huwakumbusha wakati wa swala na kubaini muelekeo wa Qibla huku ikiwa pia na uwezo kutambua misikiti iliyokaribu. Aplikesheni hiyo inahitaji mtumizi kuwasha mfumo wa GPS au location data kubaini aliko.

Salaat First 5.1.13 for Android - Download

Kwa mujibu wa taarifa, aplikesheni hiyo imekuwa ikiuza taarifa za watumizi kwa shirika moja la Ufaransa liitwalo Predicio, ambalo kimsingi hufanya kazi za udalali kuuza taarifa za watumizi kwa wanaozitaka. Mashirika ya usalama ya Marekani ambayo hununua taarifa za watumizi kutoka Predicio ni pamoja na FBI na ICE. Aplikesheni hiyo ya Salaat First ina watumizi zaidi ya milioni 10.  Hivi karibuni pia jarida la Vice lilifichua namna ambavyo aplikesheni ya Muslim Pro, yenye watumizi zaidi ya milioni 100 imekuwa ikiuzia Jeshi la Marekani taarifa za watumizi Waislamu.

3473688

captcha