IQNA

Aplikesheni ya Muslim Pro yakanusha kushirikiana na jeshi la Marekani

22:53 - November 18, 2020
Habari ID: 3473372
TEHRAN (IQNA) – Aplikesheni maarufu ya Kiislamu inayojulikana kama Muslim Pro imekanusha taarifa kuwa inashirikiana na Jeshi la Marekani katika kutoa taarifa za siri za Waislamu wanaoitumia katika simu zao za mkononi.

“Taarifa katika vyombo vya habari kuwa Muslim Pro inaliuzia Jeshi la Marekani taarifa binafsi za watumizi wake si sahihi na si kweli,” wasimamizi wa aplikesheni hiyo wamesema katika tovuti yao.

Shirika hilo limesema aplikesheni hiyo ina watumizi karibu milioni 100 duniani katika nchi zaidi ya 216 na inafungamana na suala la kulinda na kuhifadhi taarifa binafsi za watumizi.

Muslim Pro huwa na nyakati za swala za maeneo yote duniani na pia huweza kumuonyesha Mwislamu mwelekeo wa qibla mbali, Qur'ani Tukufu na huduma zingine muhimu za Kiislamu.

Aplikesheni ya Muslim Pro imekosolewa vikali baada ya uchunguzi uliofanywa na jarida la Motherboard kubaini kuwa aplikesheni hiyo ni miongoni mwa zingine nyingi ambazo hupokea fedha mkabala ya kuuza taarifa za walipo watumizi na kati ya wanaotumia taarifa hizo ni Jeshi la Marekani.

Muslim Pro hushirikiana na shirika la X-Mode ambalo imebainika kuwa limekuwa likiwafuatilia watu milioni 25 ndani ya Marekani na wengine milioni 40 kwingineko duniani na kuuza taarifa za watu hao. Muslim Pro imesema itasitisha ushirikiano wake na X-Mode.

Katika taarifa, X-Mode imeliambia jarida la Motherboard kuwa ushirikiano wake wa kibiashara na Jeshi la Marekani ni wa kimataifa na unahusiana na maudhui tatu ambazo ni ‘vita dhidi ya ugaidi, usalama wa mtandaoni na kutabiri muelekeao wa maambukizi ya COVID-19.”

Aplikesheni nyingine ya Kiislamu inayoshukiwa kushirikiana na Jeshi la Markeani ni Muslim Mingle.

Watumizi wa Muslim Pro katika mitandao ya kijamii wamebainisha hasira zao kuwa taarifa zao zimekuwa zikikabidhiwa Jeshi la Marekani na hivyo wameamuzi kufuta aplikesheni hiyo katika simu zao.

3936007

captcha