IQNA

21:00 - February 09, 2021
Habari ID: 3473635
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo amezindua mpango wa kitaifa wa chanjo ya corona ambapo amempongeza Waziri wa Afya Daktari Saeed Namaki kwa kumdunga mwanae wa kiume chanjo ya kwanza kabisa.

Akiashiria nukta hiyo, Rais Rouhani ambaye amezindua zoezi hilo kwa njia ya mawasiliano ya video amesema: "Wananchi wanapaswa kupata hakikisho kuwa, iwapo chanjo itaingia nchini, viongozi wa serikali wanaiamini na tuko tayari kuhakikisha kuwa wananchi wana imani na chanjo."

Rais Rouhani amemshukuru waziri wa afya kwa jitihada zote ambazo amezifanya kwa ushirikiano na wafanyakazi wa sekta ya afya katika vita dhidi ya corona.

Ameongeza kuwa ni furaha kubwa kuwa wakati huu wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kumezinduliwa mpango wa kitaifa wa chanjo.

Akimhutubu Waziri wa Afya, Rais Rouhani amesema: "Ukweli kuwa mtoto wako kipenzi alikuwa wa kwanza kupata chanjo hii ya corona ni ujumbe kuwa hii chanjo ni ya kuaminika. Iwapo wananchi wanataka tuanze ili waiamini, basi maafisa wote wa serikali wako tayari. Jana usiku niliwaambia marafiki kuwa niko tayari kuwa mtu wa kwanza kupata chanjo hii." 

Rais Rouhani ameelezea matumaini kuwa chanjo hii na chanjo zingine zote zitaingia nchini na hapo baadaye pia chanjo zilizotegenezwa hapa nchini zitaanza kutumika ili watu wote waweze kuchanjwa katika awamu hii ya kukabiliana na corona.

Waziri wa Afya Ddaktari Namaki amesema wafanyakazi wa hospitali 635 za kiserikali na za sekta binafsi nchini ambazo zinawahudumia wagonjwa wa corona watapata chanjo hiyo.

Amesema awamu ya pili ya chanjo ya corona itaanza kwa kuwalenga wale wenye magonjwa sugu na wazee na kisha baada ya hapo wananchi wengine wa kawaida watachanjwa.

3953059

Kishikizo: iran ، chanjo ، corona
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: