IQNA

Sheikh Isa Qassim
11:39 - February 14, 2021
Habari ID: 3473650
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain amesema jitihada za taifa hilo la Kiarabu katu hazitazimwa na dhulma na ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya usalama vya utawala wa kiukoo unaoingoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma.

Sheikh Isa Qassim amesema hayo katika mkutano uliofanyika usiku wa kuamkia leo katika mji mtakatifu wa Qum hapa nchini Iran, kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa 10 tokea uanze mwamko wa wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa Aal Khalifa nchini humo.

Ameeleza bayana kuwa, hakuna kingine wananchi wa Bahrain wanachokitaka ghairi ya uhuru, uadilifu, kukomeshwa ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.

Sheikh Isa Qassim amesisitiza kuwa, ukandamizaji huo hata kwa kutumia majeshi ajinabi kama ya Saudia hautawanyamazisha Wabahrain na kwa ari na shauku kuu wataendelea kupigania haki zao.

Kadhalika mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu ameutaka utawala wa Aal Khalifa uwaachilie huru wafungwa wote wa kisiasa nchini Bahrain. 

Mwamko wa watu wa Bahrain dhidi ya utawala wa kifalme ulianza Februari 14 mwaka 2011, na ungali unaendelea licha ya utawala huo dhalimu kushadidisha ukandamizaji na utumiaji mabavu dhidi ya wananchi hao wanaotaka mabadiliko.

Tokea Februari 14 mwaka 2011 hadi sasa utawala wa Aal Khalifa umewakamata na kuwafunga jela zaidi ya raia 11,000 kwa visingizio mbali mbali visivyo na maana. 

3473969

Kishikizo: Bahrain ، Isa Qassim
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: