IQNA

Waislamu wa Bahrain

Utawala wa Bahrain walaaniwa kwa kumkamata mwanazuoni mkubwa wa Kishia

16:31 - May 25, 2023
Habari ID: 3477043
TEHRAN (IQNA)- Kukamatwa Sheikh Muhammad S'anqur, Alimu mashuhuri, Khatibu na Imamu wa Sala ya Ijumaa wa Msikiti wa Imam Sadiq (AS) ulioko katika kitongoji cha Al-Diraz nchini Bahrain kumeibua moto wa hasira za umma wa Waislamu nchini humo.
Katika miaka kadhaa ya karibuni, mamlaka za utawala wa Bahrain zimewatia nguvuni shakhsia na wanazuoni wengi wa kidini, wakiongozwa na Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Al-Wifaq na kuwahukumu vifungo jela kwa sababu za kisiasa.
Jana Jumatatu, maafisa wa Bahrain walimkabidhi kwa ofisi ya mwendesha mashtaka kwa ajili ya uchunguzi wa jinai Sheikh Muhammad S'anqur, Imamu wa Ijumaa wa Msikiti wa Imam Sadiq (AS) katika eneo la Al-Diraz la Waislamu wa madhehebu ya Shia wa nchi hiyo. 

Kwa mujibu wa chaneli ya Al-Mayadeen, Jamil Kadhim, afisa wa Jumuiya ya Kiislamu ya Al-Wifaq nchini Bahrain, ameeleza katika taarifa aliyotoa hapo jana kwamba Sheikh S'anqur ni miongoni mwa wanazuoni wahakiki na watafiti wanaotajika wa fikra za Kiislamu na akabainisha kuwa alimu huyo ni mtoaji mahubiri ya misimamo ya wastani ya mageuzi ya kisiasa na anachofikiria ni maslahi ya nchi, watu, amani na usalama tu.

Jamil Kadhim ametaka Sheikh S'anqur aachiliwe huru akisisitiza kuwa mwanazuoni huyo ni mdhamini wa usalama na mtetezi wa haki na uadilifu nchini Bahrain.
Raia wengi wa Bahrain nao pia wamelaani kukamatwa kwa Sheikh S'anqur na mamlaka za usalama na kusambaza katika mtandao wa Twitter ujumbe wa hashtagi "#simamisha_unyanyasaji_wa kikoo", unaoonyesha kuwa kushikiliwa kwa alimu huyo kumetokana na sababu za kikoo na kikabila.
Wakati huo huo, maeneo kadhaa ya Bahrain yameshuhudia maandamano ya hadhara ya kulaani kutiwa nguvuni Sheikh S'anqur, ambapo waandamanaji wametaka mwanazuoni huyo aachiliwe huru na kukomeshwa maudhi na manyanyaso ya kikabila ambayo wananchi wa Bahrain wanakabiliana nayo.
Idara Kuu ya Upelelezi na Ushahidi wa Jinai ya Bahrain imedai kuwa hotuba za Sala ya Ijumaa za Sheikh S'anqur "zina ukiukaji wa sheria, ikiwa ni pamoja na kuwatusi viongozi, na kwamba eti zinachochea waziwazi chuki na dharau za kimakundi."
Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al-Wifaq ya Bahrain nayo pia imesisitiza kuwa, viongozi wa Bahrain wanatekeleza kwa makusudi siasa na sera za maudhi na manyanyaso ya kidini nchini humo na kwamba hatua kali hizo zimeshtadi baada ya vuguvugu la mapinduzi ya Februari 14, 2011.

/3483693

captcha