IQNA

Sri Lanka yaendeleza chuki dhidi ya Uislamu yatangaza marufuku ya niqab, yakufunga shule 1,000 za Kiislamu

20:43 - March 14, 2021
Habari ID: 3473732
TEHRAN (IQNA)- Katika kile kinachoonekana ni mwendelezo wa kushtadi chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Sri Lanka, serikali ya nchi hiyo imetangaza kuwa karibuni hivi itapiga marufuku uvaaji wa vazi la staha la burqa (niqabu) ambalo huvaliwa na baadhi ya wanawake wa Kiislamu.

Kadhalika serikali hiyo imetangaza kuwa inajiandaa kufunga madrasa na shule za Kiislamu zaidi ya elfu moja nchini humo kwa madai kuwa zinatoa mafunzo yenye misimamo iliyofurutu ada.

Katika kikao na waandishi wa habari jana Jumamosi, Sarath Weerasekera, Waziri wa Usalama wa Umma nchini humo alisema amesaini waraka ambao unasubiri baraka za Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kupiga marufuku vazi hilo la stara.

Amedai kuwa, "enzi zetu huko nyuma wasichana na wanawake hawakuwa wakivalia niqab, uvaaji huu wa sasa ni alama ya kuibuka misimamo ya kidini iliyochupa mipaka. Hakuna shaka tutapiga marufuku vazi hilo kwa maslahi ya usalama wa taifa."

Aidha serikali ya Colombo hiyo jana ilitangaza kujipa mamlaka mutlaki ya kuwakamata na kuwazuilia washukiwa wa ugaidi kwa muda wa hadi miaka miwili kwa ajili ya 'kuwavua' misimamo iliyofurutu ada, kwa kutumia sheria tata ya kupambana na ugaidi.

Hivi karibuni, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ilionyesha wasi wasi wake kutokana na kushtadi chuki dhidi ya jamii ya Waislamu nchini Sri Lanka na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuwadhaminia usalama Waislamu hao.

Hivi karibuni,  kufuatia mashinikizo, serikali ya Sri Lanka imebatilisha uamuzi wake wa kuteketeza moto miili ya Waislamu waliopoteza maisha kutokana na Corona au COVID-19.

Sri Lanka ina jamii ya watu milioni 21.8 inayoyajumuisha watu wa makabila na dini tofauti huku wafuasi wa dini ya Budha wakiunda zaidi ya asilimia 70 ya jamii yote ya nchi hiyo ya Asia Kusini. Kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Colombo, Waislamu wanaunda asilimia 9 tu ya jamii yote ya nchi hiyo.

3474232

 

Kishikizo: sri lanka waislamu
captcha