IQNA

Samia Suluhu aapishwa kuwa rais wa Tanzania

15:59 - March 19, 2021
1
Habari ID: 3473746
TEHRAN (IQNA)- Bi. Samia Suluhu Hassan mapema leo asubuhi, saa nne asubuhi kwa majira ya Afrika Mashariki ameapishwa kuwa rais wa 6 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ameapishwa katika hafla ndogo iliyofanyika katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar pamoja na viongozi wengine mbalimbali wa nchi hiyo.

Mara baada ya kuapishwa Rais Samia Suluhu Hassan amepigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalumu kwa mara ya kwanza akiwa amirijeshi mkuu wa majeshi ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Katika hotuba yake ya kwanza akiwa Rais wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwito wa umoja na mshikamano kwa Watanzania wote.

Bi. Suluhu ni rais wa kwanza mwanamke katika eneo la Afrika Mashariki ni pia ni miognoni mwa viongozi wachache Waislamu wa kike duniani wanaovaa vazi la staha la Hijabuu.

Bi Suluhu ni rais wa sita wa Tanzania na anachukua nafasi ya Dk John Magufuli aliyefariki dunia  Machi 17,  2021. Magufuli amefariki kutokana na matatizo ya moyo ikiwa imepita miezi michache baada ya kuanza muhula wake wa pili kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, nafasi ya urais inapokuwa wazi kwa sababu yoyote ikiwemo kifo, viongozi watatu wameorodheshwa na ni Makamu wa Rais, na endapo hatakuwepo atachukua Spika wa Bunge na kama hayupo atachukua Jaji Mkuu.

Hivyo kwa mujibu wa katiba, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan amechukua nafasi rais wa Tanzania na atakamilisha kipindi kilichosalia cha rais aliyaga dunia.

 

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa rais wa awamu ya sita, Rais Samia Suluhu Hassan amesema hakuna kitakachoharibika.

 

"Amenifundisha mengi na amenilea na kuniandaa vya kutosha, tumepoteza kiongozi shupavu. Alikua chachu ya mabadiliko"Rais Samia amesema.

 

Rais pia alieleza pia kwa hisia namna ambavyo kuchukua kwake hatamu kumekuwa kugumu kwake.

"Leo nimekula kiapo cha juu sana nikiwa na majonzi tele na kukiwa na simanzi kubwa mtaniwia radhi leo nitaongea kwa uchache sana mengine tutazungumza"

Aidha Rais Samia amewataka Watanzania kuzika tofauti zao.

"Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa, kufarijiana kuonyesha upendo, undugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na utanzania wetu."

 

''Si wakati wa kutazama yaliyopita lakini ni wakati wa kutazama yaliyo mbele. Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu. Huu si wakati wakutazama mbele kwa mashaka bali kwa matumaini.si wakati wa kunyosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono," Rais Samia ameeleza.

3960651

Imechapishwa: 1
Inatathminiwa: 0
Haiwezi kuchapishwa: 0
Nching'wa N Shaaban
0
0
I'm very happy to read your new,keep it up
captcha