IQNA

Kiongozi Muadhamu amteua Mohseni-Ejei kuwa mkuu wa Idara ya Mahakama Iran

16:01 - July 01, 2021
Habari ID: 3474061
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amemteua Hujjatul Islam wal Muslimin Gholamhossein Mohseni-Ejei kuwa Mkuu mpya wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika dikrii, Ayatullah Ali Khamenei amemtaka Mohseni-Ejei kutazama kwa makini dhamira na malengo ya Idara ya Mahakama kama yalivyoainishwa kwenye Katiba ya nchi, sambamba na kuendelea kufuata njia ya mageuzi.

Kiongozi Muadhamu amemuasa Mkuu mpya wa Vyombo vya Mahakama vya Iran kutumia teknolojia mpya kufanikisha shughuli za taasisi hiyo, na vile vile kuwateua shakhsia wachapakazi na waaminifu.

Kadhalika Ayatullahi Khamenei amemtaka Mohseni-Ejei kuendeleza kwa nguvu vita dhidi ya ufisadi mbali na kuwa na mtagusano na mawasiliano ya moja kwa moja na wananchi.

Hujjatul Islam wal Muslimin Gholamhossein Mohseni-Ejei ambaye alikuwa Naibu Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, anakuja kurithi mikoba ya Rais mteule wa Iran, Hujjatul Islam Walmuslimin Ebrahim Raeisi.

Sayyid Ebrahem Raeisi alitangazwa mshindi katika kinyang'anyiro cha urais cha Juni 18 mwaka huu, kwa kupata kura karibu milioni 18 za wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu.

3475117

captcha