IQNA

Kongamano la London lajadili 'Amani kwa Mtazamo wa Qur'ani'

17:24 - July 10, 2021
Habari ID: 3474088
TEHRAN (IQNA) - Kongamano la 14 la Umoja wa Kiislamu limefanyika London, Uingereza Ijumaa Julai 9.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, mada ya kongamano la mwaka huu ilikuwa ni 'Nafasi ya Thamani za Kibinadamu Katika Kufikia Amani ya Dunia kwa Mtazamo wa Qur'ani Tukufu."

Akizungumza katika kongamano hilo Hujjatul Islam wal Muslimin Hamid Shahriari Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesmea pasina kuwapo umoja, umma wa Kiislamu hauwezi kufikia malengo yake ya kupata nguvu na ustawi.

Ameashiria umuhimu wa thamani za pamoja za ubinadamu ambazo chimbuko lake ni Fitra na kisha akaashiria aya ya 30 ya Sura al Rum isemayo: " Basi uelekeze uso wako kwa dini iliyo sawa sawa ndilo umbile Mwenyeezi Mungu alilowaumba watu. Hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe wa Mwenyeezi Mungu, hiyo ndiyo dini iliyo haki lakini watu wengi hawajui."

Hujjatul Islam Shahriari ameashiria pia aya ya 28 ya Sura al Baqarah isemayo: "Mnamkataaje; Mwenyeezi Mungu na hali mlikuwa wafu naye akawahuisheni, kisha atawafisheni, kisha Atawahuisheni, kisha mtarejeshwa kwake."

Ameongeza kuwa leo kuna mirengo miwili duniani; mmoja ni ule wa wanaodai kutetea haki za binadamu lakini wakati huo huo wanamwaga damu na kueneza udhalimu na ufisadi duniani kwa jina la kutetea demokrasia, uhuru na haki za binadamu na mrengo wa pili ni ule unaopambana na hao madhalimu na maadui wa ubinadamu.

Aidha amesema amani na utulifu hauwezi kupatikana duniani iwapo misingi ya Kiislamu haitatekelezwa.

3982967

captcha