IQNA

Mkutano wa Umoja wa Kiislamu kwa njia ya intaneti Afrika Kusini

14:21 - October 22, 2020
Habari ID: 3473285
TEHRAN (IQNA) – Kituo cha Utamaduni cha Iran huko Pretoria, Afrika Kusini kimepanga mkutano wa umoja wa Kiislamu kwa njia ya intaneti maarufu kama webinar.

Bw. Ahmad Ali Muhsinzade, Mwambata wa Utamaduni wa Iran nchini Afrika Kusini, amesema hafla hiyo itakuwa sehemu ya Mkutano wa 34 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu.

Amsema kikao hicho kitafanyika Oktoba 30 kwa njia ya intaneti kutokana na vizingiti vivlivyowekwa vya mijumuiko wakati huu wa janga la COVID-19.

Muhsinzadeh amesema mada kuu katika webinar hiyo itakuwa ni kujadili 'Ushirikiano wa Kiislamu Wakati wa Maafa na Majanga.

Ameongeza kuwa, Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madehehebu za Kiislamu itashirikiana pia na vituo vya utamaduni vya Iran nchini Zimbabwe na Tanzania katika kuandaa mkutano huo.

Mapema mwezi huu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu Hujjatul Islam Hamid Shahriyari alisema Shahriari amesema sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa Umoja wa Kiislamu zitafanyika 29 Oktoba sawa na 12 Rabi ul Awwal na kumalizika 3 Novemba sawa na 17 Rabi ul Awwal.

Hujjatul Islam Shahriyari amesema kwa kuzingatia kuwa ulimwengu unakabiliwa na janga la corona, mwaka huu mada ya mkutano wa umoja wa Kiislamu itakuwa ni kuhusu ushirikiano wa Kiislamu wakati wa majanga na maafa.

Amesema ushirikiano wa nchi za Kiislamu katika kukabiliana na corona ulikuwa tafauti na nchi za Magharibi. "Waislamu duniani, hasa watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wameonyesha wanaweza kukabiliana na janga hili kwa ustaarabu huku katika nchi za Magharibi kukishihudiwa matatizo mengi hasa utamaduni wa kiliberali wa ubinafsi," amesema Hujjatul Islam Shahriyari.

Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu hufanyika kila mwaka kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW.

Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shiia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

3930558

captcha