IQNA

14:22 - July 17, 2021
News ID: 3474107
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema, uhusiano na ushirikiano imara baina ya Chuo cha Kidini cha Qum na cha Al Azhar cha Misri unaweza kuwa na matokeo chanya na yenye faida kwa Waislamu duniani katika kupambana na ukufurishaji na misimamo ya kufurutu mpaka.

Hujjatul-Islam Hamid Shahryari ameeleza hayo katika kongamano la kimataifa la “Mchango wa Vituo vya Kielimu na Kiutamaduni katika Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu” kilichofanyika mjini Tehran kwa njia ya mawasiliano ya video. Amesema Uislamu unawatambua Waislamu wote kuwa ni ndugu; na kwa kufanya hivyo kuimarisha uhusiano wa upendo kati yao; na akaongeza kwamba, kutoa mwito wa kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu hakumaanishi kuchanganywa madhehebu zote na kuwa na madhehebu moja tu, lakini maana hasa ya kukurubiana ni madhehebu zote kuishi kwa masikilizano bila taasubi na uadui kati yao.

Hujjatul-Islam Shahryari ameashiria pia fatua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu uharamu wa kuyavunjia heshima matukufu ya Waislamu wa Kisuni na akaeleza kwamba, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ameharamisha kuyavunjia heshima matukufu ya madhehebu za Shia na Suni.

Katika hotuba yake hiyo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amegusia baadhi ya nukta kuhusu uhusiano wa chuo cha kidini cha Qum na cha Al Azhar na akasema: uhusiano na ushirikiano madhubuti baina ya taasisi mbili hizi unaweza kuwa na matokeo yenye faida katika Ulimwengu wa Kiislamu na kwa Waislamu, ikiwemo katika suala la kupambana na ugaidi, misimamo ya kufurutu mpaka, ukufurishaji, mauaji, kuepusha vita, kutatua tofauti kati ya nchi za Kiislamu, kuimarisha uhusiano kwa ajili ya kuzuia kuvunjiwa heshima matukufu ya madhehebu mbalimbali, kuepusha madhehebu kuzushiana mambo ya uongo na kukabiliana na mitandao ya habari inayochochea tofauti na mifarakano baina ya madhehebu za Kiislamu.

3984465

 

Tags: iran ، al azhar ، waislamu ، qum ، shahriyari ، madhehebu
Name:
Email:
* Comment:
* captcha: