IQNA

Wanajeshi 14 wa Syria wauawa katika hujuma ya kigaidi Damascus

23:17 - October 20, 2021
Habari ID: 3474449
TEHRAN (IQNA)- Televisheni ya taifa ya Syria imetangaza kuwa askari 14 wa jeshi la nchi hiyo wameuawa na wengine watatu wamejeruhiwa katika shambulio la bomu lililolenga basi lililokuwa limebeba askari hao mapema leo.

Shambulio hilo la kigaidi la leo asubuhi lililotokea wakati watu wengi walipokuwa katika hekaheka za kuelekea makazini na mashuleni ni la maafa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa miaka kadhaa sasa mjini Damascus tangu vikosi vya serikali vilipovikomboa vitongoji vya mji mkuu huo wa Syria kutoka kwenye makucha ya makundi ya kigaidi.

Duru za jeshi la Syria zimelieleza shirika la habari la nchi hiyo SANA kuwa, mabomu mawili yaliripuka wakati basi lililobeba askari hao lilipokaribia daraja la Hafidh al-Assad na jengine la tatu liliteguliwa na kitengo cha uhandisi cha jeshi.

Kwa mujibu wa duru hizo, mabomu hayo yalikuwa yametegwa ndani ya basi lenyewe.

Kamanda wa Polisi wa Damascus Meja Jenerali Hussein Jumaa amelielezea shambulio hilo la kigaidi kuwa ni la "kiwoga" na kuwatolea mwito wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama endapo watagundua au kuona kitu chochote cha kutia wasiwasi.

Hali ya utulivu imetawala katika mji mkuu wa Syria Damascus kwa miaka kadhaa sasa na mashambulio kama hayo ni nadra kutokea. Shambulio la mwisho lilitokea mwaka mmoja uliopita, wakati Mufti wa Kisuni wa mkoa huo, Adnane al-Afyouni, alipouawa katika mripuko wa bomu lililotegwa katika gari lake. Lakini shambulio hili lilitokea huko Qoudsaya, kitongoji cha karibu na Damascus.

4006650

Kishikizo: syria damascus magaidi
captcha