IQNA

Maoni

Hujuma ya kigaidi ya Daesh dhidi ya Haram ya Shah Cheragh

17:50 - August 16, 2023
Habari ID: 3477448
TEHRAN (IQNA)- Takriban miezi 10 baada ya shambulio la kigaidi la mwaka jana kwenye Haram Takatifu ya Hadhrat Ahmad bin Musa (AS) maarufu kama Shah Cheragh mjini Shiraz kusini mwa Iran, magaidi walishambulia tena eneo hilo takatifu siku ya Jumapili, na matokeo yake yakawa ni kuuawa shahid waumini wawili na wengine wanane kujeruhiwa.

Mnamo Oktoba 26, 2022, gaidi mwenye silaha aliingia ndani ya eneo hilo la ibada, na kuwaua wafanyaziara 15, wakiwemo wanawake na watoto, na kujeruhi wengine kadhaa kabla ya kupigwa risasi na kujeruhiwa na vikosi vya usalama. Wahusika wa kitendo hicho cha kigaidi walinyongwa mwezi uliopita.

Kundi la magaidi wakufurishaji wa Daesh au ISIS limedai kuhusika na hujuma zote mbili.

Hujuma nyingine ya  kigaidi ya Jumapili  huko Shah Cheragh inaweza kuchukuliwa kuwa ni jaribio jipya la maadui la kulenga usalama wa jamii na pia kudhoofisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, jaribio ambalo limekuwa likifanywa katika miaka ya hivi karibuni katika fremu ya vita vya kisaikolojia dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Hivi ni vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambavyo vimeanzishwa na vinaendelezwa na Marekani na utawala wa Kizayuni na baadhi ya waungaji mkono wao katika ulimwengu wa Magharibi na eneo la Asia Magharibi.

Kuzusha milipuko ya vurugu kama vile vitendo vya kigaidi nchini Iran  na kuvuruga usalama wa jamii na usalama wa kisaikolojia wa wananchi ni mojawapo ya mipango ya maadui ya kutaka kuzuia udumishwaji wa amani na utulivu nchini Iran.

Katika hali ambayo machafuko ya mwaka jana ambayo yalianza kwa uchochezi na mipango maalumu ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu yalisitishwa kutokana na kuwa macho wananchi na hatua za vyombo vya usalama na pia njama za kuigawa nchi vipande vipande na kueneza machafuko zilisambaratishwa, sasa kwa mara nyingine tena maadui, kwa shambulio la kigaidi la Shah Cheragh, wameonyesha kwamba ili kufikia malengo yao maovu, wanaendelea kutisha na kuua watu, haswa katika maeneo ya kidini.

Lengo jengine linalofuatiliwa na magaidi na waungaji mkono wao ni kujaribu kuonyesha kuwa serikali ya Iran imeshindwa kudumisha usalama, kwa sababu kuendelea kwa mashambulizi ya kigaidi na ukosefu wa usalama wa jamii kunaweza kuvuruga amani ya kisaikalojia ya wananchi, na matokeo yake ni kuwafanya baadhi ya watu kuamini kuwa mfumo wa Kiislamu unaotawala Iran hauna uwezo unaohitajika wa kudumisha usalama nchini.

Ahmad Vahidi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Jumapili asubuhi alifika katika eneo la tukio hilo na kusema: "Hujuma ya kigaidi  katika Haram ya Hadhrat Ahmed bin Musa (AS) imefanywa na maadui wakubwa wa Iran, na iwapo maadui wa Jamhuri ya Kiislamu wanadhania kuwa wanaweza kuhatarisha usalama na uthabiti wa nchi kwa vitendo hivyo vya uoga na kuwafyatulia risasi watu, basi, wamekosea kwa sababu taifa la Iran liko imara.”

Nukta nyingine muhimu ni kimya na kutochukua hatua taasisi za kimataifa na serikali za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu katika kukabiliana na matukio ya kigaidi nchini Iran. Ukimya wa jumuiya ya kimataifa na hasa nchi zinazodai kutetea haki za binadamu kuhusu hujuma za kigaidi dhidi ya Iran ni ishara ya undumakuwili na ni sababu kuu za kuendelea mashambulizi ya kigaidi na kwa msingi huo, madola hayo ya Magharibi ni waungaji mkono wa vitendo vya ugaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Muhammad Jaradat, mtafiti wa Kipalestina, katika makala aliyoandika katika tovuti ya Televisheni ya Al Mayadeen chini ya  anuani ya "Hujuma dhidi ya Shiraz ya ISIS (Daesh), Mashambulio ya Umwagaji damu katika Maeneo ya Ibada" , alisisitiza kuwa njia pekee ya kukabiliana na njama za Marekani na utawala wa Kizayuni za kuzusha fitna kati ya Sunni na Shia kwa kutumia Daesh Waislamu wote kuwa naumoja. .

Ameongeza kuwa: "Kundi la kigaidi la Daesh linaakisi mafundisho ya kidini na kisiasa ambayo yameliruhusu kukabiliana  wapinzani wao  kwa namna ambayo pia imeacha mshtuko mkubwa wa kihisia na kisaikolojia.

Uzoefu wa zaidi ya miongo mine baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu unaonesha kuwa, maadui daima wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali zikiwemo za ugaidi, machafuko, ghasia na kutumia mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi ili kuzuia kufikiwa fikra na malengo ya mapinduzi hayo ili kuudhoofisha mfumo wa Kiislamu  na kuzuia ustawi na  maendeleo ya Iran. Bila shaka, kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu: "Wanajaribu kutumia njia zote kutekeleza njama  dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, lakini kwa sababu mahesabu yao yamekuwa na makosa, wameshindwa hadi sasa na watafeli katika siku zijazo."

4162883

Kishikizo: shah cheragh magaidi
captcha