IQNA

Bunge la Iran lalaani uamuzi wa Uingereza kuhusu Hamas

13:55 - November 20, 2021
Habari ID: 3474583
TEHRAN (IQNA)- Sekretarieti ya Kudumu ya Mkutano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina Katika Bunge la Iran imelaani vikali hatua ya serikali ya Uingereza ya kuiweka Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS katika orodha ya makundi ya kigaidi.

Taarifa ya sekretarieti hiyo imeeleza kuwa, hatua hiyo ya Uingereza inakinzana wazi kabisa na haki za binadamu.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Sekretarieti ya Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina imesema kuwa, hapana shaka kuwa kitendo hicho cha watu waoga ambacho ni mwendelezo wa usaliti wa Tangazo la Balfour katika fremu ya  kuendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina, kuwafanya wakimbizi mamilioni miongoni mwao na kuwaua maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wasio hatia wa Kipalestina.

Kwa upande wake Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) nayo imetoa taarifa ya kulaani uamuzi uliojaa chuki wa serikali ya Uingereza wa kuiweka harakati hiyo katika orodha ya 'makundi ya kigaidi.'

Sehemu moja ya taarifa ya Hamas imeeleza kuwa, "inasikitisha kuona kuwa Uingereza inaendeleza ujinga wake wa huko nyuma ambapo badala ya kuliomba radhi taifa la Palestina na kurekebisha makosa yake ya kihistoria iwe ni katika kutangaza azimio chungu la Balfour au ukoloni wake Palestina na kisha kuikabidhi ardhi hii kwa Wazayuni, sasa inaunga mkono uvamizi wa maghasibu dhidi ya taifa linalodhulumiwa la Palestina."

Hamas imeitaka Uingereza isitishe mara moja uungaji mkono kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na imetoa wito kwa watu huru duniani na waungaji mkono wa Palestina kulaani vikali uamuzi huo wa Uingereza.

4014687

captcha