IQNA

Yemen yatekeleza hujuma ya kulipiza kisasi dhidi ya UAE

22:56 - January 17, 2022
Habari ID: 3474819
TEHRAN (IQNA)- Ndege 20 zisizo na rubani pamoja na makombora 10 ya balestiki ya Jeshi na Kamati za Kujitolea za Wananchi wa Yemen yameshambulia maeneo muhimu na nyeti ndani ya ardhi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Shambulio hilo limetokea leo Jumatatu ambapo kwa mujibu wa ripoti hiyo, Jeshi la Yemen kwa kushirikiana na Ansarullah limeshambulia ndani kabisa ya ardhi ya UAE kwa kutumia ndege 20 zisizo na rubani na makombora 10 ya balestiki. Taarifa zinasema kuwa, kwa uchache watu watatu wameuawa na wengine 6 kujeruhiwa katika shambulio hilo la kulipiza kisasi.

Shambuio hilo limefanyika ndani ya mji mkuu wa UAE yaani Abu Dhabi na moshi pamoja na miale ya moto imeonekana ikielekea juu baada ya mashambulio hayo.

Kabla ya hapo, Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree aliuonya Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa uache kuuwa wananchi wa Yemen vinginevyo San'a italipiza kisasi kwa nguvu zake zote ndani ya ardhi ya Imarati.

Kabla ya kuenea habari hii pia, msemaji huyo wa Jeshi la Yemen alikuwa ameahidi kutangaza habari muhimu kuhusu operesheni maalumu iliyofanywa na Wayemen ndani ya ardhi ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mchana wa leo Jumatatu shirika la habari la Imarati WAM limetangaza habari ya kutokea miripuko miwili karibu na maghala ya mafuta na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abu Dhabi, mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ikishirikiana na UAE na kwa himaya ya Mareakni na utawala haramu wa Israel na madola mengine ya magharibi ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Vita vilivyoanzishwa  na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen na kuendelea hadi sasa vimeshapelekea mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha, mbali na kuwaacha wengine milioni nne wakiwa hawana pa kuishi. Aidha vita hivyo vimesababisha matatizo mengi ya ukosefu wa chakula, matibabu na elimu kwa watu wa Yemen.

Uchokozi na uvamzi wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen umebomoa na kuharibu zaidi ya asilimia 85 ya miundombinu ya nchi hiyo masikini zaidi katika Bara Arabu na kuisababishia pia uhaba mkubwa wa chakula na dawa.

Katika kulipiza kisasi jinai hizo, Jeshi la Yemen hutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maeneo ya kistratijia ya Saudi Arabia na UAE.

/3477415

Kishikizo: yemen saudi arabia uae
captcha