IQNA

Buriani, Sheikh Abdillahi Nassir, mwanazuoni nguli wa Kiislamu Afrika Mashariki

17:10 - February 12, 2022
Habari ID: 3474921
TEHRAN (IQNA) - Januari 11 2022 ilikuwa siku ya huzuni kwa Waislamu wa Afrika Mashariki na Ulimwengu wa Kiswahili kwa kuondokewa na Sheikh Abdillahi Nassir, aliyekuwa mwanazuoni nguli wa Taaluma za Kiislamu na lugha yetu aushi ya Kiswahili.

Kifo kimetunyanganya mwanazuoni huyu wa daraja ya juu ambaye alisifika kwa kujenga hoja na kuwa mbali na malumbano yasiyo na staha akibebwa na khalifiya ya kuwa mwanazuoni nguli wa Kisuni Afrika Mashariki kabla ya kuingia katika madhehebu ya Shia Ithnasheri miaka ya 80.

Kifo ni maendeleo kwa maana ya mabadiliko yanayomtoa mwanadamu kutoka katika hali moja hadi nyingine. Moja ya maana ya kifo ni kutengana Roho na mwili baada ya kuunganishwa kwa njia ya kupuliziwa roho katika mwili pale mimba inapofikisha arobaini ya tatu au siku mia na ishirini toka ilipotungwa.

Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani na Aali Zake) ameuelezea mchakato huu wa makuzi ya mimba katika Hadith kutoka kwa Swahaba Abuu Abdir-Rahmaan Abdillaah bin Mas-uud (Allaah Amridhie) ambaye amesema: “Ametusimulia Mjumbe wa Allaah (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arobaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arobaini zijazo huwa ni donge la damu, kisha arobaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho (yake).  Na huamrishwa maneno manne; Kuandika riziki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, na (ni) mtu muovu au mwema. WALLAAHI! naapa kwa Yule Ambaye hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye amali za watu wa Peponi (Jannah) hadi ikawa baina yake na Pepo (Jannah) ni dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa motoni akaingia motoni. Na mmoja wenu hufanya amali za watu wa motoni hadi ikawa baina yake na moto ni dhiraa na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa Peponi (Jannah) akaingia Peponi (Jannah)” [Hadith hii inapatikana katika vitabu cha Hadith za Mtume Muhammad viitwavyo Sahih Al-Bukhary na Sahih Muslim]

Tunafundishwa hapa kuwa kifo si kuangamia kwa roho bali kutengana roho na kiwiliwili chake kama tukio hilo linavyotokea kwa kila mmoja wetu pale anapolala.

Tunasoma katika Qur’an Tukufu Sura ya 39 (Surat Az-Zumar), Aya ya 42 kuwa: “Mwenyeezi Mungu huzipokea roho zinapokufa. Na zile zisizokufa (huzipokea) wakati wa kulala kwake, huzishika zilizohukumiwa kufa, na huzirudisha nyengine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.”

Kufa kwa roho hapa ni kule kutengana na kiwiliwili chake ili kutimiza ule muda wa uhai na maisha ya mwanadamu duniani. Roho haifi bali huonja utengano baina yake na kiwiliwili - Kila nafsi (roho) huonja umauti.

Mwanadamu ana umauti wa aina mbili na uhai wa aina mbili. Kabla ya roho kupulizwa katika mwili pale mimba inapotimiza siku mia na ishirini mwanadamu anahesabiwa kuwa katika hali ya umauti (Umauti wa Kwanza), roho ikipulizwa anauanza uhai wa kwanza hadi pale anapoufikia Umauti wa Pili, tunaoujua sana, ili afikie Uhai wa Pili, wa mwisho na wa milele.

Tunasoma katika Qur’an Tukufu Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah), Aya ya 28 kuwa: “Vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa wafu, akakufufueni! Kisha atakufisheni, tena atakufufueni, kisha kwake mtarejeshwa?”

Kwa nini leo tunazungumzia kifo?

Siku ya Jumanne ya tarehe 11 Januari mwaka huu 2022 ilishuhudia kutangulia kurudi kwa Mola wetu Mlezi mmoja wa wanazuoni wa daraja la juu ambaye uanazuoni wake katika taaluma za Kiislamu na lugha ya Kiswahili hautiliwi shaka, Sheikh Abdillahi Nassir.

Alifariki mjini Mombasa, nchini Kenya na kuzikwa katika maziyara (makaburi) ya Wakilindini, Mombasa Alasiri ya Siku hiyo hiyo ya Jumanne tarehe 11 Januari mwaka huu wa 2022.

Hadi anafariki, Marehemu Sheikh Abdillahi Nassir alikuwa mwanazuoni mbobezi wa Kishia, mwalimu, mhadhiri na mwandishi maarufu wa Kiislamu aliyeandika mengi yenye manufaa katika Taaluma za Dini ya Uislamu na lugha ya Kiswahili.

Marehemu Sheikh Abdillahi Nassir amefariki akiwa na umri wa miaka 89 na kwamba pamoja na umri huo mkubwa amefariki akiwa anaendelea kuandika Tafsiri ya Qur’an Tukufu kwa  lugha ya Kiswahili aliyoifanyia kazi sehemu kubwa ya maisha yake ikiwemo kuwa mhariri wa lugha hiyo katika shirika la uchapishaji la Oxford Universitry Press, jijini Nairobi, Kenya.

Sheikh Abdillahi Nassir ni nani?

Marehemu Sheikh Abdillahi Nassir alizaliwa Mombasa tarehe 1 Juni 1932. Alijiunga na madrasa kwa ajili ya mafunzo ya awali ya Dini ya Uislamu akiwa na umri wa miaka 4 mnamo mwaka 1936 na kuendelea hadi mwaka 1946. Kadhalika alisoma shule ya msingi ya Arab Boys Primary School mwaka 1941 hadi mwaka 1949 kabla ya kwenda Zanzibar kujiunga na Chuo cha Ualimu cha Bet El Ras Teacher Training College mwaka 1950 hadi mwaka 1951.

Aliporudi Mombasa alifundisha shule ya msingi ya Arab Boys Primary School hadi mwaka 1954 alipolazimika kuacha kazi kwa sababu ya kuumwa, Alipopata nafuu alijiunga na chuo cha Mombasa Institute of Muslim Education akiwa karani wa hesabu na mwalimu wa muda wa dini katika chuo hicho na hayo ni mwaka 1955 hadi mwaka 1957.

Ikumbukwe kuwa marehemu Sheikh Abdillahi Nassir alijitumbukiza katika siasa za kudai uhuru wa Kenya kati ya mwaka 1957 na mwaka 1963  ambapo alichaguliwa katika Baraza la Kenya la Kutunga Sheria ambapo alihudumu kati ya mwaka 1961 hadi mwaka 1963 na alihudhuria mkutano wa kihistoria kuhusu Katiba ya Kenya uliofanyika Lancaster House, jijini London, nchini Uingereza mwaka 1963.

Mwaka 1964 hadi mwaka 1965 marehemu Sheikh Abdillahi Nassir alihudumu akiwa msimamizi wa lugha ya Kiarabu na Kiswahili katika shirika la utangazaji la BBC katika ofisi zake za Nairobi, Kenya.

Baadaye mwaka 1965 hadi mwaka 1973, Sheikh Abdillahi Nassir alijiunga na kuhudumu katika shirika la Oxford University Press, akiwa mhariri wa Kiswahili katika ofisi yake ya Nairobi, Kenya.

Mwaka 1973 marehemu Sheikh Abdillahi Nassir aliachana na shirika la Oxford Universitry Press na kuasisi kampuni yake ya uchapishaji – Shungwaya Publishers Limited.

Mwaka 1974  Shirika la Oxford University Press lilimuajiri marehemu Sheikh Abdillahi Nassir kuwa meneja mkuu wa ofisi yake ya Nairobi ambapo alihudumu kati ya mwaka 1974 hadi mwaka 1977.

La kuzingatia ni kuwa marehemu Sheikh Abdillahi Nassir aliyeshiriki harakati za siasa za kudai uhuru wa Kenya, mara tu baada ya uhuru wa Kenya aliachana na mambo ya siasa kwa sababu ya kutoridhishwa na mwenendo wa siasa za Kenya wakati huo.

Historia inashuhudia kuwa marehemu Sheikh Abdillahi Nassir baada ya yote hayo yaliyoelezwa alijikita katika shughuli za dini akisomesha, akiandika makala mbalimbali na kutoa mihadhara katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuwa mwakilishi wa Afrika Mashariki wa Shirika la kidini lenye makao makuu yake nchini Saudi Arabia – World Assembly of Muslim Youths.

Katika upande wa lugha ya Kiswahili, marehemu Sheikh Abdillahi Nassir atakumbukwa kuwa mwandishi wa  ‘A Concise Dictionary of English – Swahili Idioms’ pamoja na kuandika vitabu mbalimbali kama vile:  ‘ Tamrini za Kiswahili : Sarufi na Matumizi (pamoja na majibu)’, ‘Shia na Qur’aan’, ‘Shia na Sahaba’, ‘Shia na Hadithi’, ‘Maulidi: Si Bidaa, Si Haramu’ na vingi vingine.

Kwa niaba ya wasomaji wa Uga wa Kiislamu, tunawapa pole ndugu na familia ya Marehemu Sheikh Abdillahi Nassir hususan nduguye Ustadh Abdilatif Abdallah, mtunzi wa diwani ya mashairi ‘Sauti ya Dhiki’ na jamii ya Shia Ithnasheri Afrika ya Mashriki kwa mauko ya mwanazuoni huyu wa kiislamu wa kupigiwa mfano katika kuzingatia majadiliano ya hoja na staha na kuepuka kuleta chuki na uhasama baina ya wafuasi wa dini mbalimbali na madhehebu mbalimbali.

Tunamuomba Allaah Mtukufu Akurehemu mja wake Sheikh Abdillahi Nassir, Mwanazuoni Mahiri Mwenye tabia njema. Sheikh Abdillahi Nassir atabakia mfano wa Mwanazuoni wa Kiislamu aliyezingatia nguvu ya hoja katika majadiliano na kuepuka kuhasimiana na kuchukiana kwa sababu ya kutofautiana mitizamo. INNAA LILLAAHI WAINNAA ILAYHI RAAJIUUN.

Imeandikwa na Sheikh Khamis Mataka ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania, Bakwata, na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.

Kishikizo: abdillahi nassir kenya
captcha