IQNA

Watu sita wauawa katika hujuma ya kigaidi ya Al Shabab huko Mogadishu, Somalia

23:39 - February 16, 2022
Habari ID: 3474935
TEHRAN (IQNA)- Magaidi wa kundi la al Shabaab wa nchini Somalia mapema leo wameshambulia vituo vya polisi na vya upekuzi katika mji mkuu Mogadishu. Kundi hilo la kigaidi limefanya hujuma hiyo huku Somalia ikijiandaa kwa uchaguzi wa rais ulioakhirishwa mara kadhaa.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, watu sita wamepoteza maisha katika mashambulizi ya leo ya al Shabaab huko Mogadishu.

Kundi la kigaidi la al Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida mara kwa mara limekuwa kilifanya hujuma na kutekeleza mashambulizi dhidi ya maeneo ya serikali na wiki iliyopita kundi hilo lililishambulia basi lililokuwa limewabeba makamisha wa uchaguzi.  

Abdiasis Abu Musab kiongozi wa al Shabaab amedai kuwa wapiganaji wao wameyashambulia maeneo ya serikali katika wilaya nne huko Mogadishu na katika eneo moja nje kidogo ya mji mkuu. 

Kufuatia hujuma hiyo ya al Shabaab Waziri wa Mambo ya Ndani wa Somalia Abdullahi Nor ameandika katika ukurasa wake wa twitter kwamba: "Magaidi wameshambulai vitongoji vya Mogadishu na  kulenga vituo vyetu vya polisi na vile vya upekuzi; vikosi vyetu vya usalama vimemsambaratisha adui." 

Abdifatah Aden Msemaji wa Polisi ya Mogadishu pia ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, magaidi wa al Shabaab wamekishambulia kituo cha polisi cha Kahda na pia kitongoji kingine cha Darusalam kaskazini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu. 

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 baada ya kuangushwa utawala wa Siad Barre. Katika miaka ya hivi hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wa Al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM wanaokadiriwa kufikia 21,000 wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 ili kujaribu kukabiliana na magaidi wa al-Shabab. Hatahivyo pamoja na vitihada hizo za kimataifa, magaidi wa al-Shabab wanaendelea kutekeelza hujuma Somalia na nchi jirani ya Kenya.

3477839

captcha