IQNA

Magaidi wakufurishaji wa Al Shabab waua watu 7 nchini Somalia

19:23 - December 31, 2021
Habari ID: 3474747
TEHRAN (IQNA)- Magaidi wakufurishaji wa al Shabab wameshambuia mji mmoja wa karibu na Mogadishu, mji mkuu wa Somalia na kuua watu wasiopungua saba.

Watu walioshuhudia wamesema kuwa, katika mapigano hayo yaliyotokea jana Alkhamisi, watu wasiopungua saba wameuawa wakati magaidi wa al Shabab walipokuwa wanapigana na askari wa serikali. 

Mapigano hayo yametokea katika mji wa Balad ulioko umbali wa kilomita 30 kaskazini mwa Mogadishu. Al Balad ni mji wa kilimo unaoyaunganisha maeneo ya Shabelle Kati na Lower Shabelle.

Habari hizo zimemnukuu muuza duka mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Hassan Nuru akisema kuwa, tulikuwa msikitini tunasali Sala ya Alfajiri tuliposikia mapigano makali yakitokea kwenye daraja. Baada ya hapo al Shabab wamewazidi nguvu askari wa serikali na kuuteka mji.

Kepteni wa jeshi la polisi, Farah Ali ameviambia vyombo vya habari kwamba kimsingi hakukuwa na askari wengi wa serikali wakati mapigano yalipotokea na watu walikimbilia majumbani mwao kujificha. Nimehesabu na kuona wanawake wawili raia wa kawaida wameuawa pamoja na askari watano wa serikali. Kuna baadhi ya maafisa wa polisi hawajulikani walipo hadi hivi sasa. Wapiganaji wa al Shabab walibakia muda mfupi tu katika huu mji. Al Shabab hawakuja katika kituo chetu cha polisi, lakini waliuteka mji wote na kuondoka bila ya kupiga doria, amesema.

Magaidi wa al Shabab wanatumia mzozo uliopo baina ya viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Somalia, kuteka kwa kasi miji mbalimbali ya nchi hiyo. Jumatatu wiki hii, Rais wa Somalia alimfuta kazi Waziri Mkuu wake kutokana na mzozo uliopo baina yao juu ya uchaguzi unaoendelea wa Bunge.

3477157

captcha