IQNA

Kongamano la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu nchini Pakistan

22:12 - March 23, 2022
Habari ID: 3475067
TEHRAN (IQNA) - Mkutano wa 48 wa siku mbili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ulianza jana Jumanne mjini Islamabad, mji mkuu wa Pakistan.

Mkutano wa 48 wa siku mbili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ulianza jana Jumanne mjini Islamabad, mji mkuu wa Pakistan.

Katika horuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan amesema: "Lengo lake kuu ni kuimarisha na kutatua matatizo ya nchi zote wanachama."

Shah Mahmood Qureshi amesema uingiliaji wa kigeni katika masuala ya nchi za Kiislamu, kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi za Waislamu duniani, kuwanyima Waislamu haki ya kujitawala, hususan katika Palestina na Kashmir, ni masuala yanayoweza kudhoofisha umoja na mshikamano wa Kiislamu na kuzusha mivutano mbalimbali.

Mkutano wa siku mbili wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa OIC mjini Islamabad ni fursa kwa wawakilishi wa nchi za Kiislamu waliohudhuria katika kikao hicho kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala muhimu ya Ulimwengu wa Kiislamu khususan kuamua namna ya kusaidia juhudi za kupunguza matatizo ya nchi za Kiislamu zilizoathiriwa na mgogoro.

Hivi sasa, mbali na kadhia ya Palestina ambayo ni tatizo la miaka mingi la ulimwengu wa Kiislamu, suala la Afghanistan na yanayojiri nchini humo ndio ajenda muhimu zaidi inayozingatiwa katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC. Disemba 19, 2021, Pakistan iliandaa mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa OIC kufuatia hali ya wasiwasi iliyojitokeza nchini Afghanistan baada ya Taliban kushika tena madarakani ya nchi hiyo. Katika mkutano huo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) walikubaliana kuanzisha mfuko wa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Afghanistan ili kukabiliana na mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa nchi hiyo, ambao umewafanya mamilioni ya watu wakabiliwe na njaa.

Kuanzishwa Mfuko wa Misaada ya Kibinadamu kwa Ajili ya Afghanistan, ambayo ni matokeo ya kikao cha awali cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa OIC, kumeibua matumaini ya kudhaminiwa baadhi ya mahitaji ya kimsingi ya wananchi wa Afghanistan na kupunguzia mashaka yao. 

Afisa wa Mpango wa Chakula Duniani, David Bezley anasema: "Karibu nusu ya wakazi wa Afghanistan wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa njaa. Waafghani wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu, na ikiwa msaada huu hautatolewa, nchi hiyo itakumbwa na janga kubwa la binadamu."

Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa OIC nchini Pakistan, unaongozwa na Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita tangu kundi la Taliban lilipotwaa tena madaraka ya Afghanistan, Iran imekuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika kutoa misaada ya kibinadamu kwa nchi hiyo na kufanya juhudi za kujenga mwafaka wa kikanda baina ya nchi jirani ili kusaidia jitihada za kurejesha utulivu na kuzuia mgogoro mkubwa zaidi wa binadamu nchini Afghanistan. Katika mkondo huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeandaa mkutano wa majirani wa nchi hiyo na kutuma shehena kadhaa kubwa za chakula, dawa na vifaa vya afya na matibabu kwa watu wa Afghanistan. 

Licha ya Marekani kufumbia jicho mashaka ya wananchi wa Afghanistan hususan kuzuiwa mali na fedha za taifa hilo,  jambo ambalo limechangia kuzidisha mgogoro wa Afghanistan, nchi wanachama wa OIC zinaweza kutoa msaada madhubuti kwa taifa hilo la Kiislamu na kuepusha mgogoro zaidi huko Afghanistan.

4044533

captcha