IQNA

Tunisia yatoa wito kwa mataifa ya Kiislamu kukomesha jinai Israel

11:06 - March 24, 2022
Habari ID: 3475072
TEHRAN (IQNA) - Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia Othman Jerandi amezitaka nchi za Kiislamu kushirikiana na kukomesha ongezeko la jinai za utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Akihutubia kikao cha 48 cha kawaida cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), waziri huyo alitoa wito kwa nchi wanachama kutekeleza wajibu wao kuhusiana na Palestina na kuacha ukiukwaji wa haki za watu wa Palestina, kwa mujibu wa Al-Alam.

Akizungumza kwa niaba ya kundi la Kiarabu, Jerandi alibainisha kuwa wanachama wa OIC wanapaswa kwa pamoja kushughulikia vitisho na changamoto mpya zinazoletwa na mabadiliko yanayofanyika kimataifa.

Ameashiria ulazima wa kudhibiti ushawishi wa mabadiliko hayo katika amani na usalama wa dunia hususan katika nchi za Kiarabu.

Waziri huyo amebainisha kuwa OIC inapaswa kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu masuala yanayoendelea kimataifa na kieneo, na kuongeza kuwa ni muhimu kuchukua hatua za pamoja za kukabiliana na ugaidi, itikadi kali za kikatili na uhalifu wa kupangwa pamoja na matokeo yake ikiwa ni pamoja na uhamiaji usiofuata utaratibu na magendo ya binadamu.

Jerandi pia alitoa wito wa kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo kwa msaada wa taasisi za fedha za Kiarabu na Kiislamu ili kukabiliana na changamoto zinazoletwa na janga la COVID-19 na mzozo kati ya Russia na Ukraine.

Akiashiria umuhimu wa kuimarisha biashara kati ya nchi za Kiislamu, waziri huyo alisema hatua hiyo inaweza kusababisha kupata uhakika wa chakula na kuendeleza sekta ya dawa.

3478258

captcha